Michezo

Amorim kupata mshahara zaidi ya maradufu Manchester United

Na GEOFFREY ANENE November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA Ruben Amorim atapokea mshahara zaidi ya maradufu amekuwa akilipwa na Sporting nchini Ureno baada ya kujiunga na mashetani wekundu wa Manchester United mnamo Ijumaa, Novemba 1, 2024.

Kwa mujibu wa taarifa nchini Ureno, Amorim amekuwa akitia mfukoni Sh416.7 milioni kila mwaka kama mshahara kambini mwa Sporting.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinaripoti kuwa United wameamua kumpa Amorim mshahara wa kati ya Sh1.0 bilioni na Sh1.1 bilioni kwa mwaka.

Amirom, 39, atajiunga na United hapo Novemba 11 kujaza nafasi ya Mholanzi Erik ten Hag aliyefutwa kazi Jumanne.

Ameratibiwa kuanza kazi November 24 wakati United watazuru washiriki wapya wa Ligi Kuu, Ipswich Town kabla ya michuano dhidi ya Bodo/Glimt (Ligi ya Uropa), Arsenal na Manchester City (Ligi Kuu) na Tottenham (Kombe la Carabao) katika usanjari huo.

Amirom amesaini kandarasi hadi Juni 2027. Kuna uwezekano wa kandarasi yake kuongezwa mwaka mmoja kutegemea matokeo.

United wamemnyakua kwa ada ya Sh1.6 bilioni kwa sababu wamemchukua kabla ya kandarasi yake kufika tamati Sporting.

Nyota wa zamani wa United Ruud Van Nistelrooy aliyekuwa naibu wa Ten Hag United, ataongoza timu hiyo dhidi ya Chelsea hapo Novemba 3.

Haijaamuliwa kama Van Nistelrooy atakuwa mmoja wa wasaidizi wa Amorim aliyechezea Benfica na Ureno kabla ya kustaafu Aprili 2017 na kutwikwa majukumu ya kocha mkuu wa Braga mwaka 2019.

Amirom alijiunga na Sporting mwezi Machi 2020 na kupata umaarufu kwa kuwa mmoja wa makocha wenye umri mdogo wanaofanya vyema barani Ulaya baada ya kuongoza klabu hiyo kutawala Ligi Kuu ya Ureno mara mbili.

Kabla ya kuelekea Old Trafford, Amorim alimezewa mate na Liverpool, Barcelona, Bayern Munich na West Ham, lakini akasalia Sporting msimu uliopita.