Habari za Kitaifa

Raila akutana na ‘makamanda’ wake walioko serikalini ODM ikitegea nyadhifa zaidi

Na JUSTUS OCHIENG November 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga Jumanne alikutana na waliokuwa wanachama wa ODM wanaohudumu katika baraza la mawaziri kwa sasa pamoja na maafisa wa chama hicho, huku nchi ikisubiri mabadiliko zaidi serikalini.

Bw Odinga alifanya mazungumzo na Mawaziri Wycliffe Oparanya (Ushirika), Hassan Joho (Madini), John Mbadi (Fedha na na Mipango ya Kiuchumi) na Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli) jijini Nairobi Jumanne usiku.

Waliohudhuria walikuwa viongozi wakuu wa chama wakiwemo; Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Mwenyekiti wa Kitaifa Gladys Wanga, Mweka Hazina Timothy Bosire na Mkurugenzi Mkuu Oduor Ong’wen miongoni mwa maafisa wengine.

Duru katika mkutano huo ziliambia Taifa Leo kwamba, ulikuwa ‘mkutano usio rasmi wa mashauriano ambao haupaswi kuibua wasiwasi wowote.

“Kama ungekuwa mkutano rasmi, vyombo vya habari vingealikwa lakini kwa vile havikuarifiwa, basi ujue hakuna chochote kilichokusudiwa kwa umma,” afisa mkuu aliambia Taifa Leo.

Bw Oparanya, aliyekuwa naibu kiongozi wa chama cha ODM, alisema Bw Odinga alikuwa “akishauriana na ‘makamanda’ wake baada ya siku nyingi nje ya nchi.”

Alikuwa nje ya nchi kwa muda kwa ajili ya kampeni zake za AUC (Tume ya Muungano wa Afrika) na hivyo alikuwa akishauriana na ‘makamanda’ wake.

Bw Oparanya alidokeza kuwa Bw Odinga aliwafahamisha kuhusu mpango wake wa kuzindua kampeni ya AUC mjini Addis Ababa ambapo anatarajiwa kufichua maono na vipaumbele vyake kwa Afrika.

“Hata alituhimiza sisi katika baraza la mawaziri kuchukua jukumu letu kwa uzito kwa ajili ya Wakenya kwa kuunga mkono sera za serikali na aliwataka maafisa wa chama kuungana kama upinzani kukosoa serikali kikamilifu,” Bw Oparanya aliongeza.