Habari za Kitaifa

Ruto alivyoponda wabunge akiwaita kizingiti katika vita dhidi ya ufisadi

Na  NDUBI MOTURI November 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto alilaumu mashirika ya serikali kwa kutibua vita dhidi ya ufisadi huku akiwashutumu wabunge kwa kuchelewa kupitisha Mswada wa kudhibiti Mgongano wa Maslahi unaolenga kuzuia ufisadi.

Dkt Ruto katika hotuba yake kwa kitaifa alilaumu Bunge la Kitaifa na Seneti kwa ‘kupuuza’ kwa makusudi vipengee muhimu vya mswada wa mgongano wa kimaslahi wa 2023 na kunyima taifa zana zinazohitajika kupambana na ufisadi.

Hotuba yake ilijiri baada ya Wakenya wakiongozwa na viongozi wa kidini kuitaka serikali kuzuia ufisadi unaofyonza rasilimali za nchi.

Mswada wa Mgongano wa Maslahi ulianzishwa mwaka jana na unalenga kuwazuia maafisa wa umma kuwa na mguu mmoja katika utumishi wa umma na mwingine katika sekta ya kibinafsi.

Kandarasi za serikali

Lakini wabunge na maseneta waliondoa baadhi ya vipengee na kuwapa maafisa wa umma wakiwemo wabunge, magavana, mawaziri, makatibu na wakuu wa mashirika ya umma idhini ya kunufaika na kandarasi za serikali.

Kiongozi wa nchi katika hotuba yake aliwashutumu wabunge hao kwa kuwa na mgongano wa kimaslahi kwa kubadilisha vifungu muhimu kwenye mswada huo.

“Pia ni jambo lisilokubalika kwa wabunge kunyima taifa chombo kinachohitajika mno katika vita dhidi ya ufisadi kwa kuendelea kuhujumu upitishaji wa Mswada wa Mgongano wa Maslahi. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, acheni kujikokota katika mswada huu isipokuwa kama kuna mgongano wa kimaslahi katika kupitishwa kwa sheria ya mgongano wa kimaslahi,” alisema.

Matamshi ya rais yanajiri siku chache baada ya kuwateua watu kadhaa mashuhuri wanaotuhumiwa kwa ufisadi. Baadhi ya walioteuliwa hivi majuzi ni pamoja na aliyekuwa gavana wa Nairobi Evans Kidero (Mwenyekiti wa Shirika la Kitaifa la Biashara la Kenya (KNTC).

Kuondoa kesi za washukiwa wa ufisadi

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma pia alilaumiwa kwa kuondoa kesi zinazowakabili watu wakubwa. Baadhi ya kesi hizo ni pamoja na kufutilia mbali mashtaka dhidi ya Gavana wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki, aliyekuwa waziri Najib Balala, na waliokuwa magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Mike Sonko (Nairobi).

“Haiwezekani kuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma anaendelea kuondoa kesi kwa sababu, kwa njia fulani, hawawezi kupata mashahidi,” alisema kuhusu kufutwa kwa kesi hizo. Rais pia alisuta mahakama kwa kucheleweshwa kesi zinazohusu ufisadi.

“Pia haiwezi kuwa kwamba washukiwa wa ufisadi hukimbilia kortini kuzuia kukamatwa. Pia hakuna sababu ya kesi za ufisadi kujivuta katika mahakama zetu kwa miaka mingi wakati mahakama zilezile zina uwezo wa kuamua kesi za uchaguzi na mizozo inayohusiana nayo katika muda wa miezi sita,” Dkt Ruto alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA