HabariMichezo

Hussein abwaga Team Nick Mwendwa kuchaguliwa rais mpya wa soka FKF

Na CECIL ODONGO December 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

HUSSEIN Mohammed alitwaa urais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Jumamosi baada ya kuibuka kifua mbele kwenye raundi ya kwanza na kumfanya mpinzani wa karibu Doris Petra kuinua mikono, katika ukumbi wa Kasarani jijini Nairobi.

Kwenye duru hiyo ya kwanza, Mohammed alijizolea kura 43 huku Petra akipata 31. Mohammed kisha akanyakua kura 67 katika raundi ya pili huku mpinzani wake katika mkumbo huo Barry Otieno akipata kura 23.

Petra alikuwa akiungwa mkono na Rais wa sasa wa FKF, Nick Mwendwa, ambaye alikuwa mgombea-mwenza wake.

Mgombea urais Doris Petra (kulia) na mgombea mwenza Nick Mwendwa wakiwasili kuwasilisha karatasi zao za uwaniaji urais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), kwa Bodi ya Uchaguzi FKF jumba la Kandanda House mjini Naairobi, mnamo Oktoba 14, 2024. Picha|Chris Omollo

Katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi, aliyekuwa Katibu wa FKF Barry Otieno alipata kura 10, Mwenyekiti wa AFC Leopards Cleophas Shimanyula akapata nne huku jagina wa soka Sammy Owino Kempes akipata kura mbili. Tom Alila alipata kura moja nao Chris Amimo na Katibu wa Gor Mahia Sam Ochola wakiondoka nunge.

Kwa mujibu wa sheria za FKF mshindi lazima angepata asilimia 50 na zaidi, ambazo ni kura 45 kati ya wajumbe 90 ambao walipiga kura.

Awali wawaniaji ambao walikuwa wakiegemea mrengo wa Mohamed walitwaa viti sita kati nane vya uwakilishi kwenye Baraza Kuu la FKF (NEC).

Mwenyekiti wa klabu ya AFC, Dan Shikanda, akipiga kura katika uchaguzi wa urais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), ulioandaliwa kwenye ukumbi wa Kasarani jijini Nairobi, Jumamosi. Picha|Chris Omollo

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi na Bodi ya Uchaguzi inayoongozwa na Hesbon Owila, Mohammed aliahidi kutekeleza yote yaliyokuwa kwenye manifesto yake baada ya kutwaa rasmi usukani katika jumba la Kandanda lililoko Kasarani.

“Imekuwa safari ndefu. Imani ambayo wajumbe wameonyesha kwa kunipa uongozi wa FKF nitaitumia kutimiza yale yote ambayo niliyaahidi,” akasema Mohammed.

Mgombea urais Hussein Mohammed (kushoto) na mgombea mwenza McDonald Mariga walipozindua kampeni yao ya urais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), mjini Nairobi mnamo Oktoba 12, 2024. Picha|Chris Omollo

Wajumbe hao 90 walioshiriki uchaguzi walijumuisha wenyekiti 46 wa FKF kaunti, 18 wa Ligi Kuu ya Soka (KPL), 10 wa Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) na 10 wa Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza wanaume. Wengine ni watatu wa Ligi ya Wanawake (KWPL), wawili wa NSL wadada na mmoja chama cha maslahi ya wachezaji.