Mvua yavuruga shughuli Kitengela na kuanika muundomsingi mbovu
MVUA kubwa ambayo imenyesha siku mbili katika Kaunti ya Kajiado ilisambaratisha shughuli za uchukuzi na biashara kwenye mji wenye shughuli nyingi wa Kitengela.
Sehemu ya barabara inayotoka mzunguko wa benki ya KCB na kichinjio kikubwa mjini humo ilijaa maji na kuzima shughuli za uchukuzi.
Jumatatu asubuhi kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara hiyo.
Kutokana na kuwa na mabomba mabovu ya majitaka, takataka zilitapakaa kote majini. Wakazi walilalamika kuwa kila mara mvua inaponyesha mjini humo, huwa kuna mafuriko makubwa na barabara huwa hazipitiki.
Baadhi ya bidhaa ambazo zilikuwa kwenye maeneo ya kibiashara nazo zilisombwa, wafanyabiashara wakipata hasara tele.
“Serikali ya Kaunti ya Kajiado imelala kazini. Sisi ni walipa ushuru lakini hatupati thamani na huduma za pesa zetu,” akalalamika George Onyango.