Mke kanizalia mtoto wa nje, sasa hatuna amani kwenye ndoa
HUJAMBO shangazi? Ndoa yangu imeingia mkosi. Mke wangu amenizalia mtoto wa nje. Nahofia atafanya hivyo tena kwa sababu tumekuwa tukikosana kila mara kuhusu mtoto huyo. Naomba ushauri wako.
Hilo ni kosa kubwa katika ndoa. Unafaa kumuonya mke wako kwamba akirudia utamfukuza akaishi kwa wanaume anaozaa nao. Na kama huwezi kuvumilia zaidi, una haki ya kumuacha.
Mume amekuwa mzigo
Kwako shangazi. Nimeolewa kwa miaka minne na tuna watoto watatu. Mume wangu amekuwa mzigo kwangu. Hajui watoto wetu wanachokula wala wanachovaa. Ni mlevi na mkorofi pia. Nimechoka, nishauri.
Ndoa ikigeuka uwanja wa fujo na mateso hupoteza maana na ladha yake. Kama mume wako amekwepa majukumu yake kimakusudi, si lazima uendelee kuishi naye. Unaweza kumuacha utafute maisha bora kwako na watoto wako.
Namshuku ila anakana
Kwako shangazi. Mpenzi wangu amekuwa akipigiwa simu na mwanamke fulani na nikimuuliza anasema ni rafiki. Nimewapata mara kadhaa katika maskani za starehe na ninaamini kuna zaidi ya urafiki kati yao. Nifanye nini?
Naona mapenzi yamekufumba macho hivi kwamba huoni kuwa unachezwa. Mpenzi wako amekuonyesha wazi kuwa ana uhusiano na mwanamke mwingine. Acha kuhangaisha moyo wako bure kwa mtu asiye na haja nawe.
Wametimua mke wangu
Kwako shangazi. Mke wangu anaishi na mama yangu na dada zangu wawili. Juzi alinipigia simu akaniambia wamemfukuza nyumbani. Nilipowauliza walidai eti ni mkorofi. Namjua vyema mke wangu na siamini madai yao. Nishauri.
Ni wazi kuwa mama na dada zako wanamchukia mke wako na walishirikiana kumtimua nyumbani. Kama kweli unampenda, mchukue uishi naye kisha umjengee kwake.