DimbaHabari

Amorim sasa amezea mate taji la Europa League

Na GEOFFREY ANENE, MASHIRIKA January 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Ruben Amorim ameanza kuona kombe machoni baada ya vijana wake wa Manchester United kujikatia tiketi ya moja kwa moja ya raundi ya 16-bora kwenye kombe la Europa League, walipobwaga wenyeji Steaua Bucharest 2-0 mnamo Alhamisi.

Baada ya kuanza kipute hicho kwa kupiga sare tatu dhidi ya Twente, Porto na Fenerbahce, Red Devils walipepeta PAOK 2-0, Bodo/Glimt 3-2, Viktoria Plzen 2-1, Rangers 2-1 na Steaua Bucharest 2-0 wakimaliza awamu ya makundi katika nafasi ya tatu na alama 18 kutoka duru hiyo ya klabu 36.

Diogo Dalot na Kobbie Mainoo walifungia United katika kipindi cha pili jijini Bucharest, Romania, katika mechi ambayo Amorim alifurahishwa na hatua ya kumjaribu Mainoo katika nafasi ya straika.

Mainoo alifanya vyema katika nafasi hiyo akichangia pasi iliyofungwa na Dalot kabla kupachika goli lake.
Red Devils watamenyana na Real Sociedad, Galatasaray, AZ Alkmaar au Midtjylland katika 16-bora. Wameepuka mchujo wa kufuzu awamu hiyo , unaohusisha timu zilizokamata nafasi ya tisa hadi 24.Kombe la

Europa sasa linaonekana kuwa lengo kubwa la United kwani wamehangaika sana Ligi Kuu (EPL). Iwapo watashinda kombe hilo basi watajikatia tikiti ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Kobbie Mainoo (kati) wa Man United akabwa na wachezaji Steaua Bucharest katika mechi hiyo Alhamisi. PICHA | REUTERS

Hali ya United chini ya Amorim haitabiriki, lakini Mreno huyo anasisitiza wana uwezo wa kutawala kombe hilo toto linalofuata UEFA.

Sioni tofauti kubwa tunavyocheza, lakini leo tulikuwa na muda wa kufikiria na kuelewa gemu. Tunapiga hatua,” alihoji Amorim na kuongeza: “Tunaweza kushinda mechi baada ya nyingine na kutwaa taji. Lazima tupiganie vikombe.”

Tottenham, ambao pia wanachechemea ligini, walitinga 16-bora ya Europa kwa kumaliza ndani ya mduara wa timu nane za kwanza wakifunga shughuli za makundi kwa kunyuka Elfsborg 3-0 mjini London.

Vijana wa kocha Ange Postecoglou walipata mabao yao kupitia Dane Scarlett, Oyindamola Ajayi na Mikey Moore katika dakika 20 za mwisho.

Moore aliweka rekodi kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kabisa kutoka Uingereza kufunga bao katika soka ya Ulaya. Alipata bao hilo akiwa miaka 17 na siku 172.

Alifuta rekodi ya jagina wa Tottenham, Jimmy Greaves, aliyekuwa mchezaji wa Chelsea wakati alifunga dhidi ya Lausanne Sport mnamo 1957 akiwa miaka 17 na siku 245.

 

MATOKEO YA EUROPA LEAGUE ALHAMISI:

Twente 1-0 Besiktas

Real Sociedad 2-0 PAOK

Steaua Bucharest 0-2 Manchester United

Nice 1-1 Bodo/Glimt

Olympiacos 3-0 Qarabag

Dynamo Kiev 1-0 Riga

Tottenham 3-0 Elfsborg

Midtjylland 2-2 Fenerbahce

Maccabi Tel-Aviv 0-1 Porto

Slavia Prague 2-2 Malmo

AS Roma 2-0 Eintracht Frankfurt

Ajax 2-1 Galatasaray

Lyon 1-1 Ludogorets

Athletic Bilbao 3-1 Viktoria Plzen

Anderlecht 3-4 Hoffenheim

Braga 1-0 Lazio

Rangers 2-1 Union Saint-Gilloise

Ferencvaros 4-3 AZ Alkmaar