ODM inavyopanga kuyeyusha ushawishi wa Ruto Magharibi
CHAMA cha ODM kimepanga kufanya kongamano kubwa katika eneo la Magharibi mwa Kenya Februari 28 ili kuimarisha uungwaji mkono huku Rais William Ruto akiendeleza juhudi za kujipatia wafuasi katika eneo hilo.
Kulingana na Naibu Kiongozi wa ODM Bw Godfrey Osotsi, kongamano hilo, litahudhuriwa na wajumbe 10,000, baada ya viongozi wa eneo hilo kufanya mkutano mwingine mjini Kakamega, Februari 9.
Mnamo Februari 27, ODM pia inatarajiwa kufanya hafla ya kufungua rasmi afisi ya chama hicho katika Kaunti ya Bungoma.
Bw Osotsi alisema kuwa lengo la kongamano la Februari 28 ni kujadili njia za kuimarisha ODM katika eneo la Magharibi.
Kongamano hilo litafanyika siku chache tu baada ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), nafasi inayowaniwa Kinara wa chama Raila Odinga.
Wapinzani wengine wa Raila ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf, na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard James Randriamandrato na kura yenyewe ni Februari 15 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Kumewa na wasiwasi kuhusu hatima ya ODM baada ya baadhi ya maafisa wa chama hicho wanaounga mkono serikali ya Rais Ruto, kudai watamuunga mkono mnamo 2027.
“Suala la sisi kushirikiana na UDA halijajadiliwa rasmi ndani ya ODM. Kila uamuzi wa ODM hupitia vikao rasmi vya chama,” alisema Bw Osotsi Jumapili.
Mikakati hii inatafsiriwa kama njama ya ODM kupunguza ushawishi wa Rais Ruto katika eneo la Magharibi, hasa baada ya ziara yake ya siku sita hivi karibuni ambapo alitoa bonasi ya Sh150 milioni kwa wakulima kama sehemu ya mpango wa serikali wa kufufua sekta ya miwa.
“Mikutano yetu italeta pamoja magavana, maseneta, wabunge, wawakilishi na maafisa watano wakuu kutoka kila eneo bunge ili kujadili mbinu za kuimarisha ODM,” alisema Bw Osotsi.
Taifa Leo ilifanya mahojiano ya kipekee na Katibu Mkuu wa ODM Bw Edwin Sifuna, ambaye alifafanua kuwa chama hicho kitaingia katika ushirikiano tu na vyama vyenye mawazo yanayofanana na sera za ODM za kuwahudumia wananchi.
“Siasa zetu wakati mwingine zinahitaji kushirikiana kimkakati na vyama vingine, lakini lazima viwe na mtazamo sawa na wetu. Vyama vya kisiasa vyenye sera zinazofanana na ODM zinajulikana. Tunapaswa kushirikiana na vyama hivyo, si wale wanaowaonea wananchi,” alisema Bw Sifuna.