China, Urusi zatetea Iran dhidi ya amri ya Trump kuhusu nuklia
BEIJING, CHINA
CHINA na Urusi jana zilisema kuwa zitasimama na Iran baada ya Amerika kuamrisha mazungumzo na nchi hiyo kuhusiana na kustawishwa kwa kiwanda chake cha kutengeneza nuklia.
Mabalozi wa Urusi na China wameiambia Amerika kuwa na heshima kwa Iran na kusisitiza kuwa kutakuwa na mazungumzo tu iwapo vikwazo vyote vya kiuchumi ambavyo Iran iliwekewa vitaondolewa.
Nchi hizo zilisema kuwa zina imani kuhusu msimamo wa Iran kuwa mpango wake wa kustawisha nuklia yake unazingatia amani na pia kwa matumizi yake ya kawi badala ya hatari jinsi ambavyo imekuwa ikidaiwa na Amerika.
Itakumbukwa kuwa mnamo 2015, Iran ilithibiti mpango wake wa kuunda zana za kinuklia na ikaondolewa vikwazo vya kiuchumi na Amerika, Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.
“Kwa sasa hoja kuu ni kuangalia kilichosababisha kuibuka kwa hali ya sasa ya kisasa, kuondoa vikwazo na kutotumia vitisho,” akasema Naibu waziri wa masuala ya kigeni wa China Ma Zhaoxu.
Hata hivyo, Rais Donald Trump aliondoa Amerika kwenye mkataba huo mnamo 2018. Wiki jana, Rais Trump alimwaandikia Kiongozi wa Dini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akipendekeza kuwe na mazungumzo kuhusu nuklia ya Iran. Amerika inalenga kuchunguza kiwanda cha nuklia Iran kuhakiki iwapo kinatengeneza silaha hatari.
Rais Trump alisema Iran ina njia mbili tu, kukubali mazungumzo na Amerika au ivamiwe kijeshi. Tayari Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amemjibu Rais Trump na kusema kuwa hawatazungumza na Amerika wakitishiwa wala hawatafuata amri zozote walizoelekezewa.
Licha ya kuonekana kutotishwa na Amerika, uchumi wa Iran unaoyumbayumba, maisha magumu na maandamano ya raia dhidi ya serikali kuyalalamikia maisha magumu, huenda ni kati ya mambo yatakayosababisha iinamie Amerika.
Imetafsiriwa na Cecil Odongo