Raila aunga magavana kuhusu Hazina ya Barabara, alaani Bunge
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga ameunga mkono magavana katika mvutano unaoendelea kati yao na wabunge na serikali ya kitaifa kuhusu usimamizi wa fedha za ujenzi wa barabara, akisema mfumo wa ugatuzi uko hatarini.
Akizungumza mjini Mombasa wakati wa Eid Baraza, Bw Odinga alikosoa wabunge kwa kutaka kudhibiti Hazina ya Kutengeneza Barabara (RMLF), akisema hatua hiyo inahujumu mamlaka ya kikatiba ya serikali za kaunti.
“Kwa nini wabunge wajenge barabara katika maeneo yao? Kazi yao ni kutunga sheria, si kusimamia barabara au kushughulikia fedha za kaunti,” alisema Bw Odinga.
“Tuheshimu Katiba na tuache kaunti zitekeleze majukumu yao ipasavyo.
”Kauli yake inajiri wakati mvutano unaongezeka kati ya Baraza la Magavana na wabunge kuhusu pendekezo la kurekebisha Sheria ya Bodi ya Barabara ya Kenya ili kuhamisha mabilioni ya fedha kutoka kwa serikali za kaunti hadi kwa serikali ya kitaifa. Magavana wametaja hatua hiyo kama hujuma dhidi ya ugatuzi.Bw Odinga alisema maendeleo ya miundombinu kama vile ujenzi wa barabara ni jukumu la serikali za kaunti na linapaswa kuachwa mikononi mwa magavana.
“Tulikubaliana na Rais Ruto kwamba, kaunti zipate Sh450 bilioni. Fedha hizi hazifai kutumiwa vibaya. Majukumu yaliyogatuliwa yanapaswa kupewa rasilmali zinazostahili,” alisisitiza.
Pia, aliikosoa serikali ya kitaifa kwa kuhusika katika miradi ambayo kikatiba ni ya kaunti kama vile ujenzi wa masoko na vituo vya afya.“Serikali ya kitaifa inafanya nini kujenga soko Majengo, Mombasa? Hilo ni jukumu la kaunti. Katiba iko wazi,” aliongeza.
Kuhusu siasa za chama, Bw Odinga aliwataka wanachama wa ODM kukumbatia umoja na utulivu kuelekea uchaguzi wa mashinani unaotarajiwa wiki ijayo.“Huu uchaguzi usiwe vita, bali mashindano ya kindugu. Sisi ni familia moja,” alisema.