Kaunti hizi 11 zinaongoza kwa magenge hatari
MOMBASA, Nairobi na Kilifi zimeibuka kama kaunti zinazoongoza kwa magenge ya uhalifu nchini, kulingana na ripoti ya 2025 iliyotolewa na Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (NCRC).
Ripoti hiyo, iliyochambua mienendo na ongezeko la magenge katika kaunti 11, ilibaini kuwa Mombasa inaongoza kwa kuwa na magenge 73 kati ya 309 yaliyotambuliwa kote nchini.
Nairobi iliorodheshwa ya pili kwa magenge 56, huku Kilifi ikifunga tatu za kwanza kwa magenge 47. Kaunti hizi tatu pekee zinachangia zaidi ya nusu ya jumla ya magenge nchini, ishara kuwa tatizo hili limekita mizizi hasa katika maeneo ya mijini na ukanda wa Pwani.
Magharibi mwa Kenya pia imeshuhudia ongezeko la magenge, ambapo Bungoma ina 27, Busia 24, na Kisumu 20. Kaunti zingine zenye idadi ya kutisha ya magenge ni Kwale (15), Kiambu (14), Machakos (12), Garissa (11) na Nakuru (10).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, magenge haya hayaongezeki tu kwa idadi bali pia kwa uwezo wao wa kupanga, kujipanga upya, na kustahimili shinikizo za maafisa wa usalama. Magenge kama Wakali Wao, Panga Boys na Chafu za Docks yamejipatia sifa mbaya Mombasa kwa ukatili wao, huku yakionekana pia kama mamlaka isiyo rasmi mitaani.
Asilimia 82.3 ya waliohojiwa, wakiwemo maafisa wa usalama na utawala, walikiri kuwa magenge yamejaa maeneo yao. Uwepo wa magenge umefikia kiwango cha juu kuonekana wazi kwa asilimia 87.6, hali inayoonyesha kuwa hayafichi tena shughuli zake.
Baadhi ya magenge kama Mungiki yamebadilisha majina na muonekano, yakijitambulisha kama Quails au Siafu na kuvaa suti badala ya mitindo ya zamani ili kukwepa kushukiwa. Mengine yamegawanyika katika vikundi vidogo, vinavyohudumu kimyakimya katika kaunti tofauti.
Ripoti inataja ukosefu wa ajira kwa vijana kama kichocheo kikuu cha uhalifu huu, ukifuatiwa na elimu duni, uraibu wa dawa za kulevya, shinikizo za rika na mifumo dhaifu ya familia. Vijana wengi wanaojiunga ni wale walioacha shule na kuingia katika uraibu au maisha ya mitaani, wakivutwa na ahadi ya pesa za haraka..
Kipengele hatari zaidi ni ushawishi wa siasa ambapo baadhi ya wanasiasa hudaiwa kufadhili, kuwalinda au kutumia magenge kwa vurugu za uchaguzi na kutisha wapinzani. Aidha, ufisadi miongoni mwa maafisa wa usalama na mfumo wa haki pia vimetajwa kuchangia ugumu wa kudhibiti tatizo hili.
Magenge haya hujihusisha na uhalifu wa hali ya juu kama uporaji, ulanguzi wa dawa, mauaji, na ukatili wa kijamii. Yamepenya katika sekta rasmi na zisizo rasmi kama uchukuzi, ujenzi, biashara ya mihadarati na hata ulinzi mitaani.
Utafiti huo ulipendekeza mikakati 16 ya kukabiliana na magenge, huku doria za polisi, ujasusi na mpango wa Nyumba Kumi zikiorodheshwa kuwa na mafanikio ya juu kwa zaidi ya asilimia 83. Hata hivyo, mipango ya kurekebisha wahalifu waliotema magenge, msaada kwa waathiriwa, na msamaha wa serikali zilipata alama za chini.
Ripoti ilihitimisha kuwa mafanikio ya kweli yatategemea mageuzi ya mfumo wa haki, uwekezaji katika elimu, ajira, na fursa mbadala kwa vijana pamoja na kuwadhibiti wanasiasa wanaohusishwa na magenge.
NCRC ilionya kuwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti kutageuza janga la magenge kuwa tatizo la kitaifa linalohujumu utawala wa sheria na amani ya kijamii.