Jamvi La Siasa

Vigogo wa siasa waingia hofu vijana wakijipanga kugombea 2027

Na  BENSON MATHEKA April 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UCHAGUZI mkuu wa 2027 unapokaribia, vuguvugu la vijana nchini limeanza kuashiria mageuzi makubwa katika ulingo wa siasa.

Kikundi kipya kinachojiita New Generation Aspirants kimetangaza azma ya kutwaa nyadhifa za uongozi na kuashiria maisha ya kisiasa ya wanasiasa wakongwe yanaelekea ukingoni.

Kulingana na wachambuzi wa siasa, iwapo vijana watafaulu kujipanga vyema na kuungana, wanaweza kusababisha mageuzi makubwa katika uongozi wa Kenya kupitia uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, viongozi wa vuguvugu hilo walitaja hali mbaya ya uchumi, ukosefu wa ajira, madeni na ufisadi kuwa sababu kuu za kujiunga na siasa za kitaifa.

“Hatuchochewi na tamaa ya madaraka, bali na hitaji la kuokoa taifa. Wakati wa vijana ni sasa, sio kesho,” alisema Lavani Mila, mmoja wa waasisi wa kundi hilo.

Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya 2019, zaidi ya asilimia 75 ya Wakenya wako chini ya miaka 35, na kundi hili limeanza kuonyesha ishara ya kutaka kuondoa kile wanakiita “ukiritimba wa kisiasa wa wazee”.

Kundi hili linaapa kutikisa mizizi ya siasa za jadi na kupambana na wanasiasa waliodumu uongozini kwa miongo kadhaa.

Baadhi ya majina ambayo vijana wametaja kuwa mfano wa siasa wanazotaka kubadilisha ni Raila Odinga (kiongozi wa ODM) ambaye amekuwa katika siasa kwa zaidi ya miaka 40 na amewania urais mara tano lakini bado ana ushawishi mkubwa kisiasa.

Wamemtaja pia kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye aliingia bungeni mwaka 1985 na amewahi kuwa waziri na makamu wa rais.

Wengine ni Rais William Ruto ambaye wanalaumu utawala wake kwa hali ngumu inayokumba nchi, ufisadi na ukiukaji wa haki zao, Musalia Mudavadi ambaye amekuwa mbunge na waziri tangu mwaka 1989, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambaye ni kiongozi wa chama cha Ford Kenya na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

“Tumeishi kuona watu wale wale wakiingia bungeni miaka 30 iliyopita hadi sasa. Wengine hata hawajawahi kuondoka serikalini. Sasa sisi kama kizazi tunasema: imetosha,” alisema John Kiarie, msemaji wa kundi hilo.

Mbali na kushambulia mitindo ya siasa za watu binafsi, vuguvugu hili pia linahoji jinsi vyama vya kisiasa vya sasa vinavyoendeshwa. ODM, Wiper, Ford Kenya, na hata UDA vinatajwa kama majukwaa ya viongozi wale wale waliokalia uongozi kwa muda mrefu.

“Vyama hivi vinatukazia pumzi. Hakuna nafasi kwa vijana isipokuwa kama wewe ni kibaraka wa mkubwa. Tunataka vyama ambavyo vinatoka kwa watu, si kwa mabwanyenye wa siasa,” alisema Winnie Nduta, mwanaharakati wa mtandaoni.

Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba kizazi cha sasa kina silaha isiyotumika na wakongwe ambayo ni mitandao ya kijamii na tekinolojia.

“Ukisikia wakisema wanajua wanachofanya usiwapuuze. Wako mbele kitekinolojia na wanajua jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii vyema na kwa ustadi na hii ndiyo sababu imetia hofu serikali ya wanasiasa wakongwe ikaanza kulaumu matumizi ya mitandao hii kwa usalama wa taifa,” asema mchambuzi wa siasa Benard Irungu.

Kundi hili linasisitiza kuwa nia yao si kuwa wasemaji tu bali watashiriki moja kwa moja katika uundaji wa sera na siasa.

“Tunaelewa shida za jamii kwa sababu tunazihisi kila siku. Tunalipa kodi bila kazi, tunamaliza shule bila ajira. Sasa tunasema: jitokeze, gombea, piga kura, badilisha Kenya,” alisema Kiarie.

Kulingana na Irungu, huku vijana wakishinikiza mabadiliko, wanasiasa wakongwe wamekuwa na mitazamo tofauti.

“Raila Odinga, kwa mfano, alikosoa harakati za vijana kwa kusema kuwa ‘mabadiliko yanahitaji uvumilivu na uzoefu’ na vijana wanapaswa kuwa na subira ili kujifunza kutoka kwa waliowatangulia. Rais Ruto na wana mikakati wake nao wanataja silaha ya vijana (mitandao ya kijamii na tekinolojia) kama tishio kwa usalama wa taifa kuashiria kuwa kizazi cha sasa kinawatia hofu kuelekea 2027,” asema Irungu.

Anasema upinzani unaonekana kuwarai vijana akinukukuu Kalonzo Musyoka akisema ‘vijana wanahitaji msaada wa viongozi wenye uzoefu ili kuhakikisha kuwa maono yao yanafanikiwa, kwani siasa ni sanaa inayohitaji mbinu za kisomi na uzoefu wa muda mrefu.’

Mchambuzi huyu anasema wanasiasa hawa wanachokiri ni kuwa vijana wanapaswa kupewa nafasi zaidi, lakini wanasisitiza kuwa uongozi ni jukumu kubwa linalohitaji uangalifu na ufahamu wa kina wa changamoto za kitaifa.

Anaunga kauli ya mhadhiri wa chuo kikuu cha Nairobi Dkt Florence Njogu kwamba vijana wana nafasi ya kihistoria ya kutikisa siasa ya Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Licha ya kukosa nguvu za kifedha, wako na ushawishi ambao itakuwa hatari kwa wanasiasa wakongwe kupuuza,” asema.