Nairobi United yaangusha Homeboyz, Gor, Seal zikitinga nusu fainali Mozzart Bet Cup
NAIROBI UNITED Alhamisi iliendelea kutesa timu za Ligi Kuu (KPL) baada ya kuipiga Kakamega Homeboyz 2-0 kwenye uga wa Dandora, Nairobi na kufuzu nusu fainali ya Kombe la Mozzartbet.
Gor Mahia na Murang’a Seal nazo pia zilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kushinda Kariobangi Sharks na Murangá Seal 3-2 na 2-0 mtawalia.
Nairobi United ndiyo timu pekee isiyo ya KPL ambayo imesalia kwenye Mozzartbet. Mabao yake dhidi ya Homeboyz yalifungwa na Isaac Omweri na Frank Ouya.
Timu hiyo inayonolewa na Nicholas Muyoti iliondoa Tusker kwenye raundi ya 32 kisha ikachapa pia KCB katika raundi ya 16. Nairobi United ndiyo inaongoza pia kwenye Supa Ligi (NSL) kwa alama 62 zikiwa zimesalia mechi tisa msimu huu utamatike.
Mkufunzi Nicholas Muyoti alisema vijana wake walijituma sana hasa kipindi cha pili ambapo waliongeza bao la pili baada ya kuwaona Homeboyz wakiwa wanatoboka sana kwenye safu ya ulinzi.
“Vijana wameonyesha kuwa kweli wanataka kombe hili pamoja na lile la NSL ili waingie KPL. Wameonyesha kweli hawaogopi timu yoyote hata iwe ya KPL na kama kocha wao nitaendelea kuwaunga mkono ili wakifanikiwa tusherekee pamoja,” akasema Muyoti.
Kocha wa Kakamega Homeboyz ambao ni washindi wa 2023, Francis Baraza aliwakemea vijana wake akisema kuwa goli la kwanza lilikuwa kosa la kipa Ibrahim Wanzala na la pili walilegea kuondoa mpira hatari langoni.
“Huwa sipendi sana kuwalaumu wachezaji wangu sana lakini kwa leo waliniangusha,” akasema Baraza.
Mabao ya Gor yalifungwa na raia wa Cameroon Patrick Essombe na Alpha Onyango kwenye mechi ambayo pia iligaragazwa ugani Dandora baadaye jioni.
Ugani Sportpesa Arena, Victor Haki alifungia Seal bao la ushindi dakika ya 77 matokeo yakiwa 2-2. Staphod Odhiambo na Joseph ‘Kajos’ Ochieng’ walikuwa wamefungia Ulinzi kisha Joe Waithira alifunga mawili; moja kwa njia ya penalti.
Katika hatua ya nusu fainali, Murangá Seal itachuana na Gor Mahia mnamo Mei 24 2024.
Nairobi itasubiri kujua mpinzani kwenye nusu fainali nyingine Mei 25. Hii kwa sababu rufaa ambayo AFC Leopards iliwasilisha kupinga hatua ya Kamati ya Mashindano Ligini kuipa Mara Sugar ushindi, bado haijasikizwa.
Leopards iliwasilisha rufaa hiyo kutokana na kutibuka kwa mechi ya raundi ya 32 kati yao na Mara Sugar ugani Jomo Kenyatta, Kisumu mnamo Machi 19. Atakayeshinda kesi hiyo atachuana na Compel kwenye raundi ya 16 kisha kuchuana na mabingwa watetezi Kenya Police katika robo fainali.
Mshindi wa robo fainali hiyo ndiye atacheza na Nairobi United kwenye nusu fainali.