Michezo

Tusker yashindwa kuchupa kileleni, ikikabwa sare tasa na Leopards KPL

Na CECIL ODONGO May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUSKER Jumamosi iliponza nafasi ya kuchupa hadi kileleni mwa msimamo wa jedwali la Ligi Kuu (KPL) baada ya kuagana sare tasa dhidi ya AFC Leopards katika uwanja wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.

Mwanadimba wa Tusker Ian Simiyu alifunga bao dakika ya 87 lakini  likafutwa baada ya msaidizi wa refa kuinua bendera kwamba alikuwa ameotea.

Tukio hilo liliwavunja mno moyo mashabiki wa mabingwa hao mara 13 wa KPL ambao walikuwa wameanza kusherehekea kile kilichoonekana kupata ushindi dakika za jioni.

Sare hiyo ina maana kuwa Tusker ina alama 52 baada ya mechi 29  ikiwa imebakia na mechi tano pekee msimu huu uishe. Viongozi Kenya Police wana alama 52 pia japo wana ubora wa mabao na huenda wakapanua uongozi wao iwapo watapiga Kariobangi Sharks Jumapili kwenye uwanja Dandora, Nairobi.

Nambari tatu Gor nao watakuwa wakivaana na Shabana ambapo ushindi utawawezesha kupiku Tusker kwenye nafasi ya pili. K’Ogalo wana alama 50 na iwapo watashindi kisha Kenya Police ipate sare au kushindwa, basi Gor itachupa hadi kileleni mwa KPL.

Alama moja ambayo Leopards ilipata kwenye ngarambe dhidi ya Tusker iliwasukuma hadi nafasi ya tano baada ya mechi 29 wakiwa na alama 42.

Katika mechi nyingine ya mapema uwanjani humo, Bandari na Bidco pia ziliumiza nyasi bure. Bandari inayonolewa na Ken Odhiambo, imekuwa ikiandamwana na matokeo duni KPL ambapo imeshinda mara moja pekee katika mechi tano.

Sare hiyo imeacha Bidco United ikiwa bado inapambana kusalia KPL kwa kuwa ipo nafasi hatari ya 16 kwa alama 28 baada ya mechi 29.

Bandari kwa upande mwingine wapo nambari nane kwa alama 40 baada ya mechi 29.

Mnamo Ijumaa, bao la Emmanuel Osoro lilisaidia FC Talanta kuichapa KCB 1-0 ugani Dandora. Osoro sasa amefunga mabao 14 kwenye KPL, bao moja nyuma ya Ryan Ogam wa Tusker na mawili nyuma ya mfungaji bora hadi sasa Moses Shumah anayesakatia Kakamega Homeboyz.

Katika mechi nyingine iliyochezwa Ijumaa, Sofapaka iliagana sare ya 1-1 na Mathare United uwanja huo huo wa Kenyatta. Chipukizi Edward ‘Ondimo’ Omondi alifungia Sofapaka huku Musa Masika akicheka na nyavu kwa upande wa Mathare United.