Mmiliki wa kiwanda cha pombe haramu Thika aingia mitini
Na LAWRENCE ONGARO
KIWANDA cha pombe ya mvinyo cha African Spirit Distillers Ltd, mjini Thika, Ijumaa kilifungwa uchunguzi dhidi yake ukiendelea, hali iliyolazimisha mmiliki wake kwenda mafichoni.
Inspekta Mkuu wa Polisi Bw Joseph Boinet, alisema kwa muda mrefu kiwanda hicho kimekuwa kikitengeneza pombe gushi huku kikikosa pia kulipia ushuru wa KRA.
Siku chache zilizopita wafanyikazi watatu wakuu wa kiwanda hicho walitiwa nguvuni baada ya kupatikana wakiendesha shughuli zao kwa njia isiyo halali.
Bw Boinett alisema Ijumaa kwamba baada ya maafisa wa upelelezi kufanya uchunguzi wao kwenye kiwanda hicho walipata vibandiko gushi 21 milioni vya KRA huku wakikwepa kulipia takribani Sh1.2 bilioni za ushuru.
“Tumepata ya kwamba mkurugenzi wa kiwanda hicho amekwenda mafichoni jambo linalofanya tushuku kuwa anategeneza bidhaa gushi. Tutahakikisha mmiliki wa kiwanda hicho anafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka,” alisema Bw Boinett.
Alisema kiwanda hicho kitakuwa chini ya ulinzi wa polisi na hakuna mtu yeyote ataruhusiwa kuingia mle ndani hadi uchunguzi kamili ukamilike.
Kamishna wa KRA kitengo cha uchunguzi Bw Githii Mburu alisema kampuni hiyo imekuwa ikifanya biashara kwa kutumia njia ya mkato.
“Tumegundua ya kwamba hawalipi ushuru wa KRA huku wakiuza pombe wakitumia vyeti gushi vya KRA.”
Alisema kemikali wanayotumia ni hatari na watalazimika kuendelea na uchunguzi ili kuharamisha biashara hiyo ya pombe.
Afisa mkuu wa upelelezi DCI Bw George Kinoti, alisema wanataka kuchunguza uhalali wa pombe ya mvinyo inayotengenezwa hapo.
“Tunataka kuelewa jinsi pombe hiyo hukaguliwa kwenye kiwango chake cha mwisho kabla ya kujazwa kwenye chupa. Na pia ni vituongapi inayopitia kabla ya pombe hiyo kuwekwa kwenye chupa,” alisema Bw Kinoti.
Alisema iwapo kutapatikana afisa yeyote wa KRA ama polisi wanaoshirikiana kwa biashara mbovu na kiwanda hicho bila shaka watanaswa bila huruma na kushtakiwa kwa mauaji kwa kuuza bidhaa haramu.
KRA ilitangaza kuwa kampuni hiyo ilianza kuchunguzwa Januari 31, 2019 na lita 312,000 za bidhaa haramu zilinaswa kwenye kampuni hiyo.
KRA ilisema kwamba kampuni hiyo ina leseni ya kutengeneza mvinyo aina ya Glen Rock, Legend Black, Blue Moon, Legend Brandy, Gypsy King na Furaha.