Makala

Utavumilia baridi kali katika siku tano zijazo, idara yaonya

Na  BENSON MATHEKA July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Idara ya Hali ya Hewa  Kenya imeshauri kwamba hali baridi na  mawingu itaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa muda wa siku tano zijazo, hadi Jumanne wiki ijayo.

Katika tahadhari yake ya kila wiki kuhusu hali ya hewa iliyotolewa Ijumaa, Julai 25, Idara hiyo imetabiri baridi kali katika maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, maeneo ya chini ya Kusini Mashariki na ndani ya Bonde la Ufa.

Kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa, maeneo hayo yanatarajiwa kuwa na viwango vya chini sana vya joto kati ya nyuzi joto 10 hadi 12 kwa kipimo cha selsiasi.

Katika eneo la Nyanda za Juu Mashariki mwa Kenya, hali hiyo ya hewa inatarajiwa kushuhudiwa katika kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka Nithi na Nairobi.

Katika maeneo ya Bonde la Ufa na Magharibi mwa Bonde la Ufa, kaunti zinazotarajiwa kuathirika ni Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok na Kericho.

Kaunti nyingine zinazotarajiwa kupata hali kama hiyo ya hewa ni Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado na Taita Taveta, pamoja na maeneo ya ndani ya Kaunti ya Tana River.

Wakati maeneo mengi ya nchi yakitarajiwa kupata baridi kali, kaunti za Kaskazini Mashariki zikiwemo Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo zinatarajiwa kubaki na hali ya joto wastani.

Kaunti za pwani — Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale — zinatarajiwa kuwa na hali ya joto la wastani, na viwango vya joto kati ya nyuzi joto 20 hadi 21 kwa siku tano zijazo.

Katika tahadhari hiyo, Idara ya Hali ya Hewa pia imeonya kuhusu uwezekano wa mvua kubwa kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa.

Mvua hiyo inatarajiwa kuanza hasa wakati wa alasiri baada ya vipindi vya mawingu na jua asubuhi.

“Hali ya baridi ya mara kwa mara na mawingu inatarajiwa kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, maeneo ya chini ya Kusini Mashariki na Bonde la Ufa,” Idara hiyo imetangaza.

Aidha, upepo mkali kutoka kusini hadi kusini-mashariki unatarajiwa kuvuma katika maeneo ya Pwani, chini ya Kusini Mashariki, Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi mwa Kenya.