Aladwa naye achemkia upinzani kuhusu afya ya Raila
MBUNGE wa Makadara George Aladwa ameuchemkia upinzani kwa kuasisi na kudhamini habari feki kuhusu afya ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Habari kuhusu afya ya Raila zilikuwa zimeshamiri kwenye mitandao ya kijamii baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kutoonekana kwenye shughuli nyingi za umma hasa za ODM za kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.
Bw Aladwa ambaye ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi aliwakashifu vinara wa upinzani Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwadhamini wanaoendeleza habari hizo alizotaka kuwa feki mitandaoni.
“Ningependa kuwaambia Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa pamoja na mabloga wao kwamba wanastahili kufikiria upya kuhusu mikakati yao ya kisiasa,” akasema Bw Aladwa.
“VIlevile ningependa kuwaambia wafuasi wa ODM na wote wanaompenda Raila kuwa kiongozi wetu yu buheri wa afya na tunajua mahali yupo na afya yake ni imara,” akaongeza mbunge huyo wa ODM.
Pia kiongozi huyo aliwataka wanasiasa wa ODM waendelee kuunga mkono Serikali Jumuishi akisisitiza kuwa hakuna vitisho ama habari feki zinazodhaminiwa ambazo zitafanya ODM iungane na mrengo wa upinzani kumpiga vita Rais William Ruto.
Kauli ya Bw Aladwa inakuja baada ya Msemaji wa Raila Odinga, Bw Dennis Onyango, kupitia sekretariati ya chama kuwakemea Mabw Gachagua, Musyoka na Wamalwa kwa kudhamini mabloga wanaoeneza habari feki kuhusu afya ya Bw Odinga.
Ingawa hivyo, viongozi hawa wa upinzani hawakuwa wamejibu madai hayo wakati wa kuchapisha habari hizi.
Bw Odinga alionekana hadharani mara ya mwisho mnamo Ijumaa alipokutana na baadhi ya viongozi wa ODM katika hoteli ya Serena. Katika kikao hicho alionekana mchangamfu na hata alipiga picha na viongozi hao akiwemo Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, Kiongozi wa Wachache Bungeni Junnet Mohamed na Mbunge wa Kisumu Mjini Magharibi Rosa Buyu.
Baadaye siku hiyo Bw Odinga alikuwa mwenyeji wa maafisa wa klabu ya Gor Mahia ambao walimtembelea nyumbani kwake mtaa wa Karen. Akiwa na Mkewe Mama Ida, Bw Odinga alikabidhiwa jezi ya msimu mpya ya Gor naye klabu ikatoa taarifa kuwa ilipokezwa Sh10 milioni na mbunge huyo wa zamani wa Langáta.
Taarifa ya sekretaria ya Bw Odinga ilisema waziri huyo mkuu yuko nje ya nchi na iwapo angekuwa anaugua, angewafahamisha Wakenya jinsi alivyofanya alipovamiwa na corona mnamo 2021 na mnamo 2010 alipoenda kufanyiwa upasuaji nje ya nchi, wakati huo akiwa waziri mkuu.