Akili Mali

Anavyowahi masoko ya ng’ambo kwa kusindika chai ya Kenya

Na SAMMY WAWERU November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWAKA wa 2007/08, Mary Oyier alikuwa miongoni mwa Wakenya walioathirika kutokana na machafuko ya baada ya uchaguzi, tukio ambalo miaka kadha baadaye liligeuka kuwa jukwaa la ufanisi maishani mwake. 

Mary, anakumbuka jinsi alivyopoteza mali yenye thamani ya maelfu ya pesa kufuatia ghasia hizo zilizosababisha maafa na maelfu ya watu kufurushwa kutoka makwao.

“Nilikuwa nikifanya biashara ya nafaka Mombasa, na nilipoteza mali ya thamani zaidi ya Sh1 milioni,” anasema.

Aidha, Mary, alikuwa akiuza nafaka kama vile maharagwe, mahindi, mtama, wimbi na ngano, kati ya nyinginezo, ambapo alikuwa lori lililokuwa likiendea mazao Bonde la Ufa na Magharibi mwa Kenya.

Hasara aliyokadiria ilimpelekea kulemewa na msongo wa mawazo.

Chai aina ya Therapeutic ya Mary Oyier. Picha|Sammy Waweru

Katika harakati za kusaka matibabu, anakiri gharama ilikuwa ghali.

Nilijaribu dawa za hospitali na hazikunipa nafuu, kilichoniokoa ni dawa asilia – za kienyeji, Mary anasimulia.

“Dawa ya kwanza ya kienyeji Kenya ni chai tunayokuza na zaidi ya yote ikichanganywa na mitishamba, na ndiyo ilinipa nafuu, nikapona,” anaongeza mama huyo.

Akijulikana kama Mama Amani eneo la Pwani kufuatia jitihada zake kuhubiri umuhimu wa amani, Mary anasema masaibu aliyopitia na kupata tiba yaligeuka kuwa fursa ya kibiashara aliyoishia kuwekeza.

Kwenye mahojiano ya kipekee, alifichua kwamba alianza kuongeza thamani chai ya Kenya ya Gredi ya Kwanza (Grade 1) kwa kuichanganya na mitishamba kama baobab, basil, na moringa, miongoni mwa mingine, akapata nafasi katika Maonyesho ya Kibiashara na Kilimo yaliyoandaliwa na Baraza la Kitaifa la Kilimo (ASK) Mombasa, jukwaa lililofungua awamu nyingine ya maisha.

Mary Oyier aliingilia biashara ya uongezaji chai thamani baada ya kuathirika na ghasia za uchaguzi 2007/08. Picha|Sammy Waweru

“Kwa mtaji wa Sh5,000 nilisindika mseto wa chai, ambayo haikusalia wakati wa ASK Mombasa. Wanunuzi waliagiza oda zaidi,” alisema. Mengine sasa yamekuwa historia.

Miaka 15 baada ya kuathirika na ghasia za uchaguzi, Mary alianzisha Maria Agri Products, kampuni inayoongeza thamani chai ya Kenya – Grade 1 na inayovuma kibiashara Mombasa na eneo la Pwani kijumla.

Kando na kuhudumia soko la ndani kwa ndani Kenya, amepenyeza nje ya mipaka.

“Huuza bidhaa za chai Ufaransa, Netherlands, nchi za Bara Uropa, China, Somalia, Juba – South Sudan, na Burundi,” Mary anafichua.

Mjasiriamali huyu, aidha, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria makala ya 25 ya Maonyesho ya Kibiashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC MSMEs Trade Fair 2025, yaliyofanyika Uhuru Gardens, Nairobi.

Mary Oyier, mwanzilishi Maria Agri Product, kampuni ya kuchakata chai Mombasa. Picha|Sammy Waweru

Mary aliambia Akilimali kwamba kwa sasa anaunda brandi tatu za chai; therapeutic, Asian na mystic.

Akiridhia kupigwa jeki na mashirika kama Micro and Small Enterprise Authority (MSEA), SUN Business Network (SBN), Global Alliance, kati ya wengine, amewekeza kwenye mitambo na mashine ya kusaga na kukausha.

“Nilianza kwa kusindika kilo 20 kwa mwezi, na sasa ninajivunia kiwango hicho kuongezeka hadi zaidi ya 300,” akafichua.

Vipimo vyake, hupakia gramu 500 anazouza Sh1,000.

Safari ya kufikia alipo, hata hivyo, anakiri haijakuwa mteremko.

Anataja kutowa na raslimali za kutosha kuhamasisha matumizi ya chai ya Kenya iliyoongezwa thamani kwa mitishamba, mitidawa, kama changamoto kuu.