Kaunti 16 huchangia asilimia 1 ya pato la taifa
KAUNTI tano zinachangia takribani nusu ya Pato la Taifa (GDP) la Kenya, huku kaunti 16 zikichangia chini ya asilimia moja kila moja, kulingana na ripoti ya hivi punde ya hali ya ugatuzi 2025.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) inaonyesha tofauti kubwa za maendeleo ya kiuchumi kati ya kaunti mbalimbali nchini.
Kaunti tano zinazochangia asilimia 49 ya Pato la Taifa, kipimo kinachoonyesha ukubwa wa uchumi wa nchi ni Nairobi, Kiambu, Nakuru, Mombasa na Machakos.
Kulingana na ripoti hiyo, Nairobi ina mchango mkubwa zaidi wa asilimia 29.5, ikifuatiwa na Kiambu kwa asilimia 5.6, Nakuru (asilimia 5.2), Mombasa (asilimia 5.2) na Kaunti ya Machakos (asilimia 3.4).
Ripoti inaeleza kuwa utendaji mzuri wa kaunti hizi unatokana na kuwa miji na vituo vya biashara vyenye shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali.
Ripoti hiyo pia inaangazia kundi linalofuata la kaunti ambazo uchumi wake umechangia zaidi ya asilimia moja kila moja kwa pato la taifa.
Kaunti hizo ni Meru (asilimia 3), Kisumu (asilimia 2.5), Uasin Gishu (asilimia 2.4), Kilifi (asilimia 2.1), Kakamega (asilimia 2.1), Murang’a (asilimia 1.9), Bungoma (asilimia 1.9) na Nyeri (asilimia 1.9).
Pia katika kundi hilo ni kaunti za Kisii (asilimia 1.8), Narok (asilimia 1.6), Kericho (asilimia 1.6), Kajiado (asilimia 1.6), Nandi (asilimia 1.5), Bomet (asilimia 1.5), Trans Nzoia (asilimia 1.5) na Embu (asilimia 1.4).
Kaunti nyingine ni Kwale (asilimia 1.2), Migori (asilimia 1.2), Kirinyaga (asilimia 1.2), Kitui (asilimia 1.2), Homa Bay (asilimia 1.2), Nyandarua (asilimia 1.2), Makueni (asilimia 1.1), Nyamira (asilimia 1), Turkana (asilimia 1) na Siaya (asilimia 1).
Hata hivyo, licha ya baadhi ya kaunti kuonyesha matumaini ya kiuchumi, kaunti nyingine 16 kwa pamoja zilichangia asilimia 7.5 pekee ya pato la taifa.
“Kaunti nyingi kati ya hizi ni maeneo ambayo yamekuwa yakitengwa, yakikabiliwa na changamoto kama ukame, miundombinu duni na uwekezaji mdogo wa kiuchumi,” yasema ripoti hiyo.
Kaunti hizo ni Isiolo (asilimia 0.3), Samburu (asilimia 0.3), Tana River (asilimia 0.3), Lamu (asilimia 0.3), Wajir (asilimia 0.5), Mandera (asilimia 0.5), Garissa (asilimia 0.6) na Tharaka Nithi (asilimia 0.6).
Nyingine ni Marsabit (asilimia 0.6), Taita Taveta (asilimia 0.6), Pokot Magharibi (asilimia 0.7), Baringo (asilimia 0.7), Vihiga (asilimia 0.7), Busia (asilimia 0.8), Laikipia (asilimia 0.9) na Elgeyo Marakwet (asilimia 0.9).
Kulingana na ripoti hiyo, kaunti tanozinazokua kwa kasi zaidi katika sekta ya utengenezaji bidhaa ambazo ni Bomet iliyorekodi ukuaji wa asilimia 24.6, Vihiga (asilimia 25.7), Nandi (asilimia 15.2), Machakos (asilimia 15) na Pokot Magharibi (asilimia 14.8).
“Utendaji wao mzuri ulisukumwa pakubwa na upanuzi wa usindikaji mdogo wa mazao ya kilimo na kufufuliwa kwa viwanda vidogo vinavyoimarisha mifumo wa thamani ya ndani,” yasema ripoti.
Kaunti kama Busia, Laikipia, Meru na Tana River zilidumisha ukuaji thabiti wa wastani wa kati ya asilimia 8 na 12, ukichochewa na miundombinu iliyoboreshwa, upatikanaji bora wa masoko na kuongezeka kwa uwekezaji wa sekta ya kibinafsi.
Ripoti inaonyesha kuwa Nairobi, Kisumu, Nakuru na Mombasa ziliendelea kuwa nguzo kuu za uzalishaji wa kitaifa wa viwanda.
Kwa mfano, Nairobi ilirekodi ukuaji wa asilimia 8.2 mwaka 2023, huku Mombasa ikipata ongezeko kubwa la asilimia 14.8, hali inayoashiria kurejea kwa imani ya wawekezaji na upanuzi wa uwezo wa uzalishaji.
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa kaunti kama Mandera, Marsabit na Garissa zinaendelea kuinuka polepole katika sekta ya utengenezaji bidhaa, zikirekodi ukuaji wa asilimia 10.6, 9.2 na 2.8 mtawalia.
Ukuaji huo ulionekana hasa katika viwanda vinavyotegemea mifugo na utengenezaji wa vifaa vya ujenzi.
“Kwa uwekezaji endelevu katika kawi, usafiri na miundombinu ya biashara, kaunti hizi zina nafasi nzuri ya kuwa maeneo mapya ya maendeleo ya viwanda nchini Kenya,” inasema ripoti.