HabariHabari za Kitaifa

Ahadi mpya za Ruto uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia

Na CAROLINE WAFULA NA BARNABAS BII October 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto alitumia hotuba yake ya Mashujaa Dei kuorodhesha ufanisi wa serikali yake kiuchumi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, akiahidi kupunguza ushuru, kubuni nafasi zaidi za kazi kwa vijana na kuwezesha upatikanaji wa mali na teknolojia huku akitetea rekodi yake kuhusu kilimo, makazi, huduma ya afya na elimu.

Akihutubu katika Uwanja wa Kipchoge Keino, jijini Eldoret, Rais alipendekeza kuwaondolea Ushuru wa Mishahara (PAYE) wafanyakazi wanaolipwa Sh32,333 kwa mwezi, kufuta ada ya ushuru inayotozwa biashara za ardhi yenye thamani ya Sh1 milioni au chini ya kiasi hicho.

Rais alipendekeza kuondoa asilimia 25 ya ushuru unaotozwa bidhaa za kigeni kwa simu na kuunda nafasi 50,000 mpya za wanagenzi wa kulipwa kwa wanafunzi wanaomaliza vyuo kuanzia Januari 2027.

Alitangaza vilevile mipango ya kuongeza Sh5 bilioni kwenye mfuko wa Hasla Fund kabla ya mwisho wa mwaka, akitaja mikakati hiyo kuwa sehemu ya ajenda ya serikali yake kuhusu maendeleo kuanzia mashinani (BETA), aliyosema inanuiwa kuweka pesa zaidi mifukoni mwa wananchi na kuwaimarisha kiuchumi.

Hotuba hiyo vilevile ilijumuisha ujumbe wa kisiasa huku rais akiwasilisha rekodi ya utawala wake kama ushahidi wa maendeleo huku akikiri kuwa Wakenya wana haki ya kudadisi kuhusu maamuzi ya serikali yake na kuitisha huduma bora.

“Wananchi wana haki ya kuhoji serikali, kukosoa maamuzi yake na kuitisha yaliyo bora. Ni sharti tusikilize na kuwajibikia ahadi tulizotoa,” akasema Rais.

Chini ya mapendekezo mapya, wafanyakazi wanaolipwa Sh32,333 au chini ya kiasi hicho kwa mwezi wataepushiwa PAYE, hivyo kuongeza pesa wanazotia mfukoni iwapo mikakati hiyo itaidhinishwa na kutekelezwa.

Kulingana na rekodi rasmi, Kenya ina jumla ya wafanyakazi 3,468,997 walioajiriwa katika sekta rasmi.

Mpango wa sasa wa kuepusha PAYE (Sh0 – Sh24,000) unawafaidi Wakenya 1,328,625.

Hatua mpya ya kuondoa PAYE itawafaidi Wakenya wengine 362,846 na kufikisha idadi ya walioepushiwa ushuru huo kuwa 1,691,471.

Rais alisema pendekezo hilo linadhamiriwa kuzipunguzia mzigo familia zinazotaabika kukidhi mahitaji ya chakula, usafiri na matumizi mengine ya kila siku.

Pendekezo hilo limejiri huku Wakenya wakilalamikia kutozwa ushuru kupita kiasi, uwezo wa kumudu bidhaa muhimu na gharama ya maisha.

Manufaa yake halisi yatategemea taratibu za sheria na utekelezaji ikiwemo jinsi uepushaji unavyohusiana na vitengo vilivyopo vya ushuru.

Kulingana na Rais, thamani ya soko la hisa imeongezeka maradufu kutoka Sh2 trilioni hadi Sh4 trilioni, huku uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja ukipanda.

Rais alisema serikali yake imewasajili wakulima milioni 8.9 na kupunguza bei ya mbolea kutoka Sh7,500 kwa mfuko 2022 hadi Sh2,000 chini ya mpango wa mbolea ya bei nafuu.

Mifuko zaidi ya milioni 38 ya mbolea ya bei nafuu imesambazwa, alisema, na kuchangia kuongeza uzalishaji.

Alitaja kuboreshwa kwa bei katika sekta za kahawa na majanichai akisema bei ya kahawa imepanda kutoka karibu Sh70 hadi kati ya Sh110 na Sh150 kwa kila kilo.

Bei ya jumla kwa zao la majanichai imepanda kutoka Sh35 hadi Sh56 kwa kilo.

Katika sekta ya maziwa, Rais alitangaza kuwa wakulima watapokea Sh65 kwa kila lita kuanzia mwezi huu pamoja na bonasi ya ziada ya Sh2 kwa kila lita itakayolipwa kila baada ya miezi mitatu.

Alisema uzalishaji wa maziwa kitaifa umeongezeka kwa lita bilioni moja, huku bei zinazolipwa wakulima zikipanda kutoka Sh35 hadi Sh60 kwa kila lita kabla ya mabadiliko mapya.

Serikali pia ilitoa chanjo kwa zaidi ya mifugo milioni 22 na kupanua bima ya kiangazi kwenye mpango unaolenga wafugaji milioni 1.6 katika kaunti 21, alisema.

Kuhusu miundomsingi, Rais alitaja ukarabati wa barabara kuu ya Rironi-Mau Summit, kuendeleza reli ya Standard Gauge (SGR) kuelekea Kisumu na Malaba, na barabara ya Lake Victoria Ring Road.

Alitaja mipango ya kukarabati uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na kuboresha mikondo mikuu ya usafiri akihoji kuwa uwekezaji katika miundomsingi ni muhimu katika kufanikisha ukuaji kiviwanda na sekta ya kibinafsi.

Katika huduma ya afya, Rais alisema idadi ya wakenya waliosajiliwa chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) imeongezeka hadi 33.3 milioni, ikilinganishwa na milioni saba chini ya NHIF iliyovunjiliwa mbali.