Cheche ataka Starlets kuboresha safu ya ulinzi, ushambuliaji
Kocha wa Junior Starlets, Mildred Cheche, amewataka wachezaji wake kuboresha mashambulizi na kuimarisha safu ya ulinzi wanapojiandaa kukabiliana na Marekani katika Kombe la Dunia la Wanawake la chini ya miaka 17 nchini Morocco.
Kenya ilianza kampeni yake ya Kundi E kwa kichapo cha 3-0 dhidi ya China Jumatatu katika Chuo cha Soka cha Mohammed VI, Salé.
Cheche alisema wachezaji wake walionyesha kiwango kizuri katika kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kuendeleza kiwango hicho baada ya kuruhusu bao katika kipindi cha pili.
“Walijitahidi na tulikuwa na wakati mzuri katika kipindi cha kwanza hata ingawa tulikuwa tushafungwa bao moja. Katika kipindi cha pili mambo hayakuenda vizuri,” alisema Cheche.
Alisema kikosi chake kina nafasi ya kurekebisha makosa kabla ya mechi yao ya pili dhidi ya Marekani kesho katika uwanja huo huo.
“Tunapaswa kuboresha maeneo kadhaa, hasa safu ya ushambuliaji na ulinzi, ikiwa tunataka kufuzu kutoka hatua ya makundi. Tulifanikiwa kutengeneza nafasi katika eneo la wapinzani, lakini tunahitaji kuzitumia vizuri,” aliongeza.
Marekani iliweka wazi makali yake baada ya kuicharaza Samoa 17-0 katika mechi nyingine ya Kundi E Jumatatu, na hivyo kuweka warembo wa nyumbani katika mtihani mgumu wanapowania kufuzu raundi ya 16 bora.
Hata hivyo, kiungo Lindey Weey Atieno, mwanafunzi wa Raila Educational Centre jijini Nairobi, anaamini Kenya inaweza kupata matokeo mazuri.
Aliwataka Wakenya kuendelea kuwaaminia na kuwapa sapoti, akisisitiza kuwa bado ina nafasi ya kusonga mbele kwa kuwa imesalia na mechi mbili za makundi.
Weey ni miongoni mwa wachezaji watatu wa sasa waliocheza Kombe la Dunia la 2024 nchini Jamhuri ya Dominican. Wengine ni beki Brenda Awuor na mshambuliaji Faith Boke.
China ilifungua ukurasa wa mabao dakika ya 12 kupitia Xu Yue, aliyenufaika na makosa ya ulinzi wa Kenya kabla ya kupiga shuti lililojaa wavuni. Xu Xiaotang alifunga mabao mawili na kutajwa mchezaji bora wa mechi.
Kenya itamenyana na Marekani kesho kabla ya kuhitimisha mechi zake za makundi dhidi ya Samoa Oktoba 25.