Gideon afichua jinsi Ruto alivyomcheza kisiasa
MWENYEKITI wa chama cha Kanu Gideon Moi amemshutumu Rais William Ruto kwa kumdanganya na kukiuka makubaliano yao ya kisiasa, akisema alijitolea kwa manufaa ya serikali lakini baadaye akatelekezwa na kuanza kushambuliwa pamoja na familia yake.
Akizungumza nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru, Ijumaa, Bw Moi alisema alimwamini Rais na kukubali kufanya kazi naye kwa heshima ya urais, lakini ahadi walizokubaliana hazikutekelezwa.
Alifichua kuwa kabla ya Dkt Ruto kuzuru Kabarak Oktoba 10, 2025, kulikuwa na mazungumzo kadhaa yaliyolenga kupunguza mvutano wa kisiasa baina yao.
Katika mkutano huo, Rais alitangaza makubaliano ya kushirikiana na Kanu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Moi aliondoa azma yake ya kuwania tena kiti cha useneta wa Baringo, akaachia chama cha UDA kumteua mgombea wake katika uchaguzi mdogo uliofuata.
Hata hivyo, Bw Moi alisema mambo yalianza kubadilika baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga mnamo Oktoba 15, 2025.
Alisema alitakiwa kusubiri hadi serikali ikamilishe mazishi ya kitaifa ya Raila, lakini hata baada ya miezi kupita, ahadi hazikutekelezwa.
“Baada ya kifo cha Raila, niliambiwa nisubiri na kwamba makubaliano yangetekelezwa baadaye. Nilisubiri hadi Desemba, kisha Pasaka. Nilifuatilia, lakini bado nasubiri,” alisema.
Bw Moi alisema alitimiza wajibu wake kwa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha useneta, kuhakikisha Kanu haikuteua mgombea na akaahidi kumuunga mkono Rais, ikiwemo kuandaa mikutano na wazee.
Alisema hakuwahi kumuomba Rais biashara au manufaa yake ya kibinafsi, bali alitaka wataalamu kutoka jamii yake wapewe nafasi za kazi serikalini na wakazi wa Baringo wazingatiwe katika uteuzi.
“Kwenye mazungumzo haya yote, mimi ndiye niliyejitolea zaidi. Kuna watu ambao hawazungumzi nami tena kwa sababu ya makubaliano hayo; walihisi wamesalitiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa mashambulizi dhidi yake yalikuwa njama ya kuficha kushindwa kwa serikali kutekeleza ahadi ilizompa.
Bw Moi pia alimlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi kwa kutua kwa helikopta katika shamba lake Kabarak wakiwa na maafisa waliojihami kwa silaha bila ruhusa, wakati wa mazishi ya binti wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Kenya, William Ruto.
Alisema familia yake na wafanyakazi walinyanyaswa, kisha yeye akashambuliwa kwa maneno hadharani.
Pia alidai kuwa mmoja wa jamaa zake, mhariri msaidizi wa Standard Group Alex Kiprotich Chepkoit, alitekwa nyara, kuteswa na kutupwa karibu na Bwawa la Masinga.
“Nimewaambia waache familia yangu. Waache watoto wetu nje ya siasa, na kama wananitaka mimi, wanijie. Wanajua ninakoishi,” alisema.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hana uhasama binafsi na Dkt Ruto, akimtambua kama Rais wa nchi, lakini akasema amevunja makubaliano yao.
Bw Moi aliwataka wazee na wakazi wa Bonde la Ufa wamwachilie kutafuta mwelekeo mpya wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.
“Ninahitaji mambo matatu kutoka kwenu: kuniombea, kuniruhusu kuchagua njia mpya ya kisiasa na kuwaomba watu wa Baringo wanisamehe kwa kumwamini Rais Ruto na kukubali kufanya kazi naye,” alisema.
Alionya kuwa viongozi wa serikali wanaodhani wanaweza kununua uungwaji mkono wa wapigakura kwa pesa wanakosea, akisema matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou yalionyesha changamoto zinazoweza kukabili serikali mwaka 2027.
Alikosoa pia washirika wa karibu wa Rais kwa kuanza kujadili urithi wa urais wa 2032 kabla ya kuhakikisha ushindi katika uchaguzi wa 2027.
Gideon alisema kuwa uamuzi wake wa kuunga mkono Ruto ulitokana na imani kwamba makubaliano hayo yangeleta ushirikiano wa kisiasa wenye manufaa kwa wananchi, badala ya kuendeleza siasa za kushindana.
Hata hivyo, alisema amejifunza kutokana na yaliyotokea na sasa anataka nafasi ya kushauriana na wafuasi wake kuhusu mwelekeo mpya kabla ya uchaguzi wa 2027.
Aliwataka wazee wa Bonde la Ufa kumsaidia kufanya uamuzi huo kwa kuzingatia maslahi ya jamii na mustakabali wa taifa. Alisisitiza kuwa uamuzi wake hautokani na chuki dhidi ya Rais Ruto, bali ni matokeo ya kile anachosema ni kutotimizwa kwa ahadi zilizowekwa waliposuka ushirikiano huo.