Habari za Kitaifa

Wakimbizi 14,000 wa Ethiopia wakabiliwa na njaa, kiu Moyale

Na  DAVID MUCHUI, BENSON MATHEKA October 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini limesema zaidi ya wakimbizi 14,000 waliokimbia mapigano nchini Ethiopia wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi na vyoo katika eneo la Moyale, Marsabit.

Zaidi ya 10,900 wamehifadhiwa katika kambi sita huku wengine zaidi ya 4,000 wakiishi na jamaa na marafiki katika jamii.

Mkuu wa shirika hilo eneo la Upper Eastern, Malik Adan, alisema wanahitaji msaada wa dharura wa chakula, maji, vifaa vya usafi na vyoo ili kuzuia magonjwa ya kuhara.

Shirika hilo limewapa wakimbizi mahema, blanketi, mikeka, vyombo vya jikoni, huduma ya kwanza na chakula maalumu kwa watoto wadogo na akina mama.

Serikali ya kaunti ya Marsabit imeahidi kutoa mchele na maharagwe, lakini msaada huo hautoshi kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Mohamed Nane, anayesimamia kambi ya Manyatta Madrassa, alisema baadhi ya familia zinahifadhi zaidi ya wakimbizi 20 huku rasilimali zikipungua.

Alitoa wito kwa serikali na mashirika ya kibinadamu kuingilia kati haraka.

Bashir Tufa, mmoja wa wakimbizi, alisema alitoroka Ethiopia kutokana na mapigano makali kati ya vikosi vya maeneo ya nne na tano.

Alisema mapigano yanaendelea na wakimbizi hawajui watakaa Kenya kwa muda gani.