Jinsi mikutano ya kisiasa yageuka biashara nono Nyanza
SIASA katika eneo la Nyanza zinazidi kuwa ghali huku wanasiasa wakitumia mamilioni ya pesa kurai wananchi kuhudhuria mikutano yao, hali inayofanya ukubwa wa umati kuwa kipimo cha ushawishi wa kisiasa.
Nyuma ya mikutano yenye shamrashamra na viwanja vinavyojaa watu kuna biashara inayohusisha kukodisha mabasi, kutoa chakula na kulipa wanaohudhuria. Hali hii inafanya ushindani wa kisiasa kuwa mgumu kwa vijana na wagombea wasio na uwezo mkubwa wa kifedha.
Mjadala kuhusu gharama hizo ulizidi kushika kasi baada ya video ya Mwakilishi wa Wanawake wa Homa Bay Joyce Osogo Bensuda kusambaa mitandaoni, akieleza jinsi alivyopanga kutumia mamilioni ya pesa kuleta watu kwenye mkutano.
Mnamo Oktoba 2, Bensuda aliandaa Siku ya Wafanyabiashara wa Jua Kali katika Uwanja wa Raila Odinga, Homa Bay. Hafla hiyo iliwaleta pamoja wafanyabiashara kutoka wadi zote 40 za kaunti hiyo kupokea fedha na vifaa vya thamani ya Sh78.1 milioni kupitia hazina tofauti za serikali.
Katika video hiyo, Bensuda anaeleza kuwa alikusudia kutumia zaidi ya Sh1 milioni kuwalipa watu waliohudhuria, huku kila mmoja akitarajiwa kupata Sh1,000.
Alisema katika hafla nyingine ya awali alitumia mabasi 56 kusafirisha watu hadi Ndhiwa na kuwalipa waliohudhuria Sh840,000, kila mmoja akipata Sh300.
Fedha hizo hazikujumuisha gharama ya kukodi mabasi, fulana na miavuli.
Kuhusu mkutano wa uwanja wa Raila Odinga, alisema alikuwa amepanga kutumia mabasi 62 ya shule na Sh1.5 milioni kwa shughuli za kuvutia umati pekee.
Bensuda alithibitisha kuwa video hiyo ilikuwa yake, lakini akasisitiza haikuwa na uhusiano na ODM. Hakujibu maswali zaidi baada ya kutumiwa video hiyo na Taifa Jumapili.
Uchunguzi wa Taifa Jumapili unaonyesha kuwa mfumo huo unahusisha waratibu wa mashinani, vijana, waendesha bodaboda, vikundi vya wanawake na viongozi wa maoni. Wengine hulipwa fedha taslimu, huku wengine wakipatiwa nauli na chakula.
Kwa baadhi ya watu, kuhudhuria mkutano wa kisiasa kumekuwa njia ya kupata mapato ya siku moja badala ya kuonyesha tu uungwaji mkono kwa kiongozi.
Emmanuel Sirunda, mwendesha bodaboda kutoka Ugunja, Kaunti ya Siaya, ni mmoja wa wanaofaidika na mfumo huo. Alikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliohudhuria mkutano wa Rais William Ruto katika eneo la Kisumu Shipyard.
Sirunda alisema mabasi ya shule yalikodiwa kusafirisha wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya Nyanza. Walipofika, walipewa chakula na kuahidiwa malipo baada ya kusikiliza hotuba ya Rais.
“Tulipewa Sh5,000 kila mmoja, bila kujumuisha nauli na chakula cha mchana. Haya ni mapato ambayo singepata kwa siku moja,” alisema.
Zaidi ya watu 10,000 walipokea Sh5,000 kila mmoja, sawa na takriban Sh50 milioni. Kila mmoja alihitajika kuwasilisha kadi nyekundu aliyokuwa amepewa mwanzoni mwa mkutano ili kulipwa.
Shughuli ya kuzindua kaburi la kumbukumbu ya Raila Amolo Odinga mjini Bondo Oktoba 7 pia ilionyesha jinsi wanasiasa wanavyotegemea mitandao ya wahamasishaji kuvuta umati.
Sally Akinyi, jina ambalo si lake halisi, alisema amejenga mtandao wa watu anaoweza kuwaita wanasiasa wanapohitaji umati. Anasema hulipwa kuhamasisha wafuasi kwa niaba ya wabunge wawili wa Nyanza wanaotaka kuwania ugavana, mgombea wa ubunge Kisumu ya Kati na, mara nyingine, wasaidizi wa Rais Ruto.
Akinyi alisema wanaoitwa kwenye mikutano ndani ya Kisumu hulipwa Sh500 hadi Sh700, huku wanaosafiri nje ya mji wakipata kati ya Sh1,500 na Sh2,500, kutegemea kazi na umbali.
Hata hivyo, alisema biashara hiyo si ya uhakika kila wakati, kwani baadhi ya wanasiasa hushindwa kuwalipa wahamasishaji baada ya mikutano. Wakati mwingine, malipo hutolewa kupitia ufadhili wa vikundi au basari badala ya fedha taslimu.
Katika eneo la Gusii, linalojumuisha Kisii na Nyamira, viongozi wanaounga mkono serikali jumuishi huandaa hafla za uwezeshaji mara kwa mara. Baadhi ya wakazi hupokea kati ya Sh100 na Sh2,000, huku vikundi vilivyoandaliwa, kama vya wanawake na kwaya, vikivutia fedha zaidi.
Wasaidizi wa baadhi ya viongozi wanasema mikutano hii hufadhiliwa na serikali, ikiwemo utoaji wa mchele na maharagwe kwa wafuasi. Vifaa vyenye nembo za kisiasa, kama kofia na fulana, pia hutolewa.
Hata hivyo, swali kuu linalosalia ni fedha hizo zinatoka wapi na zinatolewaje.