Wanawake wanavyojichongea, waendeleza itikadi zilezile zinazowakandamiza
FATAKI
TAASUBI ya kiume inayolaumiwa kila mara kama moja kati ya visababishi vikuu vya masaibu yanayowaandama mabinti tangu jadi kwa sehemu kubwa inaendelezwa na kuchangiwa na wanawake wenyewe hadi katika kizazi hiki.
Japo ni kweli kuwa wanaume wanachangia pakubwa kuhusu ubaguzi wa jinsia ya kike, ukosefu wa usawa na mizigo wanayolazimishwa kubeba wanawake, ni muhimu kukabili ukweli mchungu kwamba mabinti, wakati mwingine, wanapigia debe na kuendeleza mifumo ileile inayowakandamiza.
Ni kinaya kwa hakika na tunaweza kufananisha uhusiano huu na mtumwa aliyezoea mateso ya mmiliki wake kiasi cha kuhiari kuendelea kumtumikia hata anapoamua kumpa uhuru wake!
Taasubi ya kiume haitamalaki kupitia matendo ya wanaume pekee bali hunawiri wakati wanawake huchunguza maamuzi ya wanawake wenzao, kuwadhalilisha mabinti wenzao kwa kukaidi matarajio ya jamii na kuwalaumu kwa majukumu yaleyale yaliyotelekezwa na wanaume.
Video iliyosambazwa sana mitandaoni iliyomwonyesha binti akimkashifu mama yake kwa kumwita ‘toxic’ eti kwa sababu alikataa kumlelea mtoto wake ili afanye kazi inatoa taswira bayana ya ukinzani huu.
Kwenye video hiyo, binti huyo anasimulia kwa machungu jinsi alivyolazimika kumwacha mtoto wake mchanga na mwanamme aliyemlazimisha baada ya mama yake kukataa katakata kurejelea majukumu ya ulezi kwa mjukuu wake.
Kiburi na matarajio yasiyo ya kirazini ya binti huyo kinastaajaisha mno kwa sababu watu waliofaa zaidi kumlea mtoto huyo basi ni wazazi wake na wala sio nyanya yake.
Hali kwamba alihisi kukomaa na kuwa tayari kujihusisha na shughuli za utu uzima ikiwemo kushiriki tendo la ndoa ni ithbati tosha kwamba alistahili kuwa tayari kwa majukumu ya utu uzima yanayojumuisha kubeba mimba, kuzaa na kumlea mtoto wake.
Badala ya kumkabili baba mtoto wake na kumshurutisha awajibike mwanamke huyu kwa maarifa au kwa kukosa maarifa alihiari kurekodi video chungunzima kumchamba mama yake kwa kutojali na kukataa kumshughulikia alipomhitaji zaidi!
Hata bila kujali kwamba mama yake sasa anastahili muda wa kupumzika baada ya kujitolea mhanga kumlea pamoja na ndugu zake, mwanamke huyu alitarajia bila soni kumtwika mwigo mwingine wa kumlelea mwanawe.