Pigo jipya kwa Ruto: korti yabatilisha agizo walimu, polisi kutengewa nyumba za bei nafuu
RAIS William Ruto amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kutangaza kuwa kinyume cha Katiba maagizo yake ya kutenga asilimia 20 ya nyumba za bei nafuu kwa walimu na maafisa wa polisi.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa walimu na polisi hawawezi kudai mgao huo wa nyumba za bei nafuu kwa kutegemea maagizo ya Rais yaliyotolewa Juni 3 na Septemba 13, 2025.
Badala yake, maombi yao yanapaswa kuzingatia vigezo vilivyowekwa katika Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu na kanuni zake, sawa na waombaji wengine.
Hata hivyo, uamuzi huo haukumaanisha kuwa walimu na polisi wamezuiwa kupata nyumba hizo. Bado wanaweza kutuma maombi, lakini hawawezi kupewa kipaumbele kwa misingi ya maagizo hayo yaliyotupiliwa mbali.
Katika uamuzi wake, Jaji Patricia Mande Nyaundi alisema Rais hana mamlaka ya kubadilisha vigezo vya kutoa nyumba vilivyowekwa na sheria.
“Maagizo ya Rais Ruto hayana nguvu za kisheria na hayawezi kubadilisha au kuongeza vigezo vya kutoa nyumba vilivyowekwa chini ya Sheria ya Nyumba za Bei Nafuu na kanuni zake,” alisema.
Jaji Nyaundi alitupilia mbali maagizo hayo akisema hayakuwa na msingi katika sheria au sera ya serikali.
Alisema ingawa serikali inaweza kuratibu utekelezaji wa sheria, haina mamlaka ya kubadilisha sheria zilizopitishwa na Bunge au kuanzisha upendeleo ambao haujatambuliwa kisheria.
Alionya kuwa kuruhusu Rais kubadilisha vigezo vilivyowekwa na sheria kungeweka mamlaka ya serikali juu ya sheria, jambo linalokiuka utawala wa sheria.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dorcas Oduor, alimwakilisha Rais, alitetea hatua hiyo akitaja Ibara ya 132(3)(b) ya Katiba inayompa Rais mamlaka ya kuratibu shughuli za wizara na idara za serikali.
Jaji alikataa hoja hiyo, akisema mamlaka hayo lazima yatumiwe kwa kuzingatia Ibara ya 10 ya Katiba, inayosisitiza utawala wa sheria, usawa, uwazi na uwajibikaji.
Alisema hakuna kifungu katika sheria inayosimamia nyumba hizo kinachowapa walimu na maafisa wa polisi kipaumbele katika kutolewa kwa nyumba hizo.
Kesi hiyo iliwasilishwa na John Maina Ndegwa na Marshalls Tito Ongoya, waliopinga maagizo hayo wakisema yalikiuka kanuni ya usawa na haki ya kila Mkenya kupata makazi inayolindwa na Ibara ya 43 ya Katiba.
Walalamishi walitaka mahakama itangaze maagizo hayo kuwa batili na kuzuia serikali kuyatekeleza, pamoja na makubaliano yaliyohusishwa na mpango huo.
Pia waliomba mahakama iamuru Bodi ya Nyumba za Bei Nafuu kuweka na kuchapisha vigezo vya utoaji wa nyumba hizo vinavyozingatia usawa na kutobagua. Walitaka pia Bunge liweke sheria au kanuni zitakazosimamia utoaji wa nyumba hizo kwa mujibu wa Katiba.
Serikali na Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) viliitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo, vikisema madai hayo yalikuwa ya jumla na hayakuwa na ushahidi wa kutosha.
Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo (KUPPET) pia kilipinga kesi hiyo. Naibu Katibu Mkuu wake, Moses Nthurima, alisema Rais alikutana na wawakilishi zaidi ya 100,000 wa walimu katika hafla ya Walimu iliyofanyika Ikulu Septemba 13, 2025.
Hata hivyo, Jaji Nyaundi alikubali kuwa kesi hiyo iliwasilishwa ipasavyo na iliibua masuala muhimu ya kikatiba. Aliidhinisha maombi ya walalamishi na kutupilia mbali maagizo ya Rais kwamba asilimia 20 ya nyumba hizo zitengewe walimu na maafisa wa polisi.
Mahakama haikuamuru upande wowote kulipa gharama za kesi hiyo kwa sababu iliwasilishwa kwa maslahi ya umma.
Akijibu uamuzi huo, Katibu Mkuu wa KUPPET, Akello Misori, alidai mahakama zinalemaza maendeleo.
“Mahakama ni maadui wa maendeleo na zimetekwa na wanaharakati. Walimu na polisi wanatozwa ushuru mkubwa na ndio wachangiaji wakuu( wa mpango wa nyumba za bei nafuu),” alisema.