HabariHabari za Kitaifa

Aliyekuwa mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki aaga dunia

Na JOSEPH WANGUI November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Kihara Kariuki amefariki dunia, akiacha nyuma historia ya zaidi ya miaka 40 katika taaluma ya sheria na utumishi wa umma.

Bw Kariuki, ambaye alihudumu kama Mwanasheria Mkuu kati ya 2018 na 2022 chini ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, pia aliwahi kuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa kwa miaka mitano.

Jaji Mkuu Martha Koome alithibitisha kifo chake Jumanne na kumtaja kama mwanasheria mahiri, kiongozi wa mahakama na mtumishi wa umma aliyechangia pakubwa katika kuimarisha taasisi za sheria nchini.

Rais William Ruto alisema mchango wake haukuishia mahakamani, bali pia ulijumuisha kuanzisha Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama (Judiciary Training Institute), iliyosaidia kuwapa majaji na maafisa wengine wa mahakama mafunzo ya kitaalamu.

Bw Kenyatta pia alimwomboleza, akisema uongozi wake katika Mahakama ya Rufaa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu uliacha alama muhimu katika taasisi za serikali.

Hata hivyo, kipindi chake kama Mwanasheria Mkuu kilikumbwa na mvutano mkubwa kati ya serikali na mahakama kuhusu uteuzi wa majaji 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Uhuru alikataa kuwateua wote, akidai alikuwa amepokea taarifa za kijasusi kuhusu masuala ya uadilifu ya baadhi yao.

Mzozo huo ulisababisha Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kutishia kumuondoa katika orodha ya mawakili kwa madai ya utovu wa nidhamu wa kitaaluma. Hata hivyo, Kariuki alipata amri ya mahakama iliyozuia hatua hiyo kwa muda.

Pia alitetea serikali kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), ambao hatimaye uliharamishwa na Mahakama ya Juu.

Kariuki alizaliwa Kiambu mwaka 1954 na kuhitimu shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 1977.

Aliwahi kuwa jaji wa Mahakama Kuu kuanzia 2003, kabla ya kuwa mkurugenzi wa kwanza wa Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama mwaka 2009.

Mwaka 2013 alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Mahakama ya Rufaa chini ya Katiba ya 2010.

Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alimuomboleza kama mwanasheria aliyejitolea katika utumishi wa umma na kuimarisha utawala wa sheria.