Habari za Kitaifa

Waendesha boda boda 300 wapata mafunzo ya usimamizi wa fedha Namanga

October 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

Takriban  waendesha boda boda 300 katika mji wa Namanga, Kaunti ya Kajiado, wamepata mafunzo ya usimamizi wa fedha ili kuwasaidia kupanga mapato yao, kulipa mikopo kwa wakati na kuimarisha biashara zao.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na kampuni ya ufadhili wa mali ya Mogo, yakilenga kuwapa waendeshaji ujuzi wa kukopa kwa uwajibikaji, kuweka akiba na kupanga bajeti kulingana na mapato yao.

Washiriki walifundishwa mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo, kuelewa viwango vya riba na masharti ya ulipaji, kutimiza makataa ya malipo na kutafuta suluhu zinazofaa wanapokumbwa na changamoto za kifedha.

Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma katika Mogo, Becky Ngigi, alisema kupata mkopo pekee hakutoshi bila kuwa na maarifa ya kusimamia fedha.

“Upatikanaji wa fedha pekee hautoshi. Watu wanahitaji pia maarifa na ujuzi wa kufanya maamuzi mazuri ya kifedha,” alisema.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa waendeshaji zana za kusimamia mapato, kutimiza wajibu wa mikopo na kukuza biashara zao kwa njia endelevu.

Mwenyekiti wa waendesha boda boda Kaunti ya Kajiado, Alex Gitari, alisema uelewa wa fedha ni muhimu kwa waendeshaji wanaotegemea mikopo kununua pikipiki na kupanua biashara zao.

Alisema waendeshaji wanapaswa kupanga mapato yao kwa kuzingatia gharama za uendeshaji, mahitaji ya familia na malipo ya mikopo.

Mafunzo hayo yanakuja wakati Kenya ikikabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaopata huduma za kifedha wanazitumia kuboresha maisha yao.

Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishaji wa Kifedha wa 2025–2028 unaonyesha kuwa asilimia 84.8 ya watu wazima nchini walipata huduma rasmi za kifedha mwaka 2024, lakini ni asilimia 18.3 pekee waliokuwa na afya nzuri ya kifedha.

Sekta ya boda boda inakadiriwa kuzalisha Sh660 bilioni kila mwaka na kusaidia zaidi ya watu milioni 2.5 kupata riziki, kulingana na ripoti ya Viffa Consult kuhusu ukuaji wa sekta hiyo.

Mogo imesema itaendelea kuunga mkono mipango inayohamasisha ukopaji wa uwajibikaji, usimamizi bora wa fedha na ukuaji endelevu wa biashara.