Habari za Kaunti

Majonzi tele mhubiri akizika wanawe 4 waliofariki ajalini Kanga

Na WINNIE ATIENO November 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WIMBI la majonzi lilitanda katika eneo la Kinango, Kaunti ya Kwale wakati Mhubiri Spencer Mdave alipokuwa akizika wanawe wanne Salem, Sharon, Sarah, na Shekinah walioaga dunia kwenye ajali katika barabara kuu ya Mombasa–Nairobi eneo la Kanga wiki mbili zilizopita.

Wanne hao walizikwa katika kaburi moja Jumatano.

Ndugu hao wanne waliaga dunia kwenye ajali iliyosababisha maafa ya watu 25 baada ya basi walimokuwa wakisafiria kutoka mazishi ya jamaa yao Lugari, Kaunti ya Kakamega kugongana ana kwa ana na lori katika eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei, Jumapili ya Oktoba 25.

Basi hilo lilikuwa limebeba abiria 50, wakiwemo jamaa wa karibu, waumini wa makanisa mbalimbali, na wachungaji 12 waliokuwa wakirejea Mombasa.

Bw Mdave, ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo, alisema alijaribu kuwaokoa wanawa lakini hakufua dafu.

“Salem, wewe ndiye mtoto wetu wa kwanza ambaye ulitufanya tukaitwa wazazi kwa mara ya kwanza. Baba yako alikuwepo eneo la ajali na alishuhudia yasiyofajirika. Alijaribu, kadri na uwezo wake kuwaokoa lakini alishindwa. Tumebaki tukitamani laiti tungefanya zaidi,” wazazi hao walisema kwenye risala yao iliyosomwa na mwana wao Shofa Mdave.

Mhubiri huyo alisema aliwaombea wanawe Sharon na Sarah, pindi baada ya ajali.

“Baba yenu aliomba nanyi, akishikilia imani na kutumaini muujiza. Alijisalimisha kwa Mungu kwa maomba si kama mchungaji, bali kama baba yenu aliyetamani kwa dhati binti zake wangeliishi,” risala ya wazazi hao ikaeleza.

Kuhusu kitinda mimba yao Shekinah, wazazi hao walilia ndoto zake zilizokatizwa kwa ghafla.

“Baba yako hakupata fursa ya kukuona eneo la ajali, lakini alibeba uchungu wa kujua kuwa umetuacha. Ni vigumu kuelewa kwa nini safari yako iliisha mapema hivi. Unasalia kuwa kitinda mimba wa familia yetu, kipenzi chetu,” wakaeleza.

Akihutubia mkusanyiko huo, Bw Mdave alieleza shukrani zake kwa majirani, waumini wa kanisa, na viongozi waliounga mkono familia hiyo wakati wa tukio hilo hadi mazishi.

“Wengi wa jamaa zangu walijeruhiwa katika ajali hiyo, na wengine waliangamia. Lakini tunamshukuru Mungu kwa sisi tulionusurika; tuko hapa kumtukuza Mungu kwa kila jambo. Siwezi kusema mengi. Nimebakiwa na watoto wanne,” alisema mchungaji huyo.

Viongozi wa kisiasa wa eneo hilo, wakiongozwa na Naibu Gavana wa Kwale Chirema Kombo, waliwapongeza mawaziri Bw Hassan Joho na mwenzake Salim Mvurya kwa kuwasaidia kifedha familia hiyo.

Katika Kanisa la ACK Mombasa Memorial Cathedral, Askofu Mkuu Alphonse Baya aliongoza ibada ya misa ya kuwakumbuka waathiriwa wengine wanne kutoka familia moja waliangamia katika ajali hiyo hiyo: Dkt Patrick Mutsunga, mke wake Younitta Mutsunga, mtoto wao Ndune Mutsunga, na ndugu yao Moses Mwadzuya.

Wanne hao walizikwa jana katika kijiji cha Mikomani, Rabai, Kaunti ya Kilifi.

Marehemu Younitta alihudumu kama mwenyekiti wa kwanza wa kamati ya mipango mkakati ya kanisa hilo mnamo 2018.

“Leo ni siku ya huzuni sana. Nimepoteza mtaalamu aliyejitolea kufanya kazi kwa ajili ya kanisa na jamii,” alisema Askofu Baya.

Alinukuu maandiko ya Biblia akiwafariji waombolezaji, Askofu Baya alinukuu Yohana 11, akikumbuka jinsi Yesu alivyolia alipowaona Maria na Martha wakimlilia ndugu yao Lazaro aliyefariki ghafla.

Kiongozi huyo wa dini alionya kuwa barabara kuu za nchini zimegeuka kuwa maeneo ya maombolezo kwa familia nyingi.

Katika mazishi na misa zote za wafu, waliohutubu walirejelea kusisitiza wito kwa serikali ichukue hatua kuepusha ajali mbaya zinazotokea mara kwa mara katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Miongoni mwa mapendekezo ni kwamba barabara ipanuliwe, na kuwe na njia tofauti ya malori makubwa ya kusafirisha mizigo.

Ajali ya Kanga ilitokea wiki chache tu baada ya nyingine eneo la Salama, karibu na Mtito Andei.