Rais Emmanuel Macron kuhudhuria kongamano UoN

Na PETER MBURU

RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye amekuwa nchini tangu Jumatano kwa ziara ya siku mbili, leo Alhamisi anatarajiwa kuhudhuria kongamano katika Chuo Kikuu cha Nairobi, katika msururu wa ziara ambazo amekuwa akifanya ndani ya nchi zinazolenga kuimarisha ushirikiano wa Kenya na taifa lake.

Rais Macron aliwasili nchini Jumatano alasiri pamoja na kundi la wafanyabiashara na maafisa wa serikali yake, ziara yake ikitarajiwa kuipa Kenya matunda ya kiutalii na uwekezaji.

Jumatano, Macron pamoja na Rais Uhuru Kenyatta waliandaa kikao na waandishi wa habari katika ikulu ya Nairobi, ambapo walieleza kuwa Kenya na Ufaransa zinalenga kuimarisha ushirikiano zaidi, haswa katika sekta za elimu, afya, usalama na utalii.

Naibu Rais Wlliam Ruto pamoja na mawaziri Amina Mohamed, Raychelle Omamo, Peter Munya, Henry Rotich, Fred Matiang’i, Keriako Tobiko, Joe Mucheru pamoja na maafisa wengine wa serikali aidha walikuwa ikulu wakati wa ziara hiyo ya Macron.

Rais Uhuru Kenyatta apiga gumzo na naibu wake William Ruto katika ikulu ya Nairobi mnamo Februari 13, 2019, wakati Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alizuru Kenya. Picha/ Peter Mburu

Kenya inatarajia kuvuna kutokana na ziara ya Macron humu nchini, ambayo imekuja na nafasi za biashara za uwekezaji na ushirikiano katika masuala mbalimbali.

Rais Macron aliahidi kuwa taifa lake liko tayari kuisaidia Kenya kukabili changamoto za kiusalama na kupambana na magaidi, mbali na kuwahimiza wafanyabiashara wake kuwekeza humu nchini.

Rais Kenyatta naye alieleza kuwa ziara hiyo ya Rais wa Ufaransa itaifaa serikali yake katika ajenda nne kuu za maendeleo ambazo inaendesha, haswa ile ya ukuzaji wa viwanda.

“Ufaransa ni mojawapo ya mataifa ambayo yamekuwa yakichangia vikubwa utalii wa nchi yetu na hivyo ziara yako kwetu inatupa moyo kuwa raia zaidi wa nchi yako watazidi kutalii humu nchini. Aidha idadi ya Wakenya wanaosafiri kwenda Ufaransa itaongezeka vilevile,” alisema Rais Kenyatta.

Uwekezaji

Rais Kenyatta alisema serikali iko tayari kuwapokea wawekezaji kutoka Ufaransa na mataifa mengine kwa ajili ya kuinua biashara humu nchini, suala ambalo Rais Macron alikumbatia, akisema hali hiyo itasaidia kuongeza nafasi za ajira kwa Wakenya.

“Sisi tuko tayari kushirikiana kwa masuala ya usalama na kukabiliana na ugaidi. Tulijadiliana kwa kina kuhusu hali ilivyo eneo hili na tutafanya kazi pamoja kuhakikisha kuna ushirikiano ili kulinda maeneo muhimu na tutaona cha kufanya na suala la Amisom Somalia,” Rais Macron akasema.

Rais huyo aidha alisema Ufaransa iko tayari kushirikiana na Kenya kuhusu masuala ya afya, elimu na kawi.

“Tunataka kuwa sehemu ya ajenda zenu za maendeleo. Tumetia saini maelewano na hata kesho asubuhi (leo Alhamisi) tutatia saini mikataba kadha ya maelewano ili kuhakikisha kuna miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoanzishwa na mingine ya maendeleo,” akasema Rais Macron.

Viongozi hao aidha kwa pamoja walizindua gari aina ya Peugot ambalo lilitengenezewa eneo la Thika humu nchini, wakisema huo ni mwanzo wa hatua nyingi za kimaendeleo zinazokuja.

Macron ndiye Rais wa kwanza wa Ufaransa kuzuru Kenya tangu ilipopata uhuru mnamo 1963.

Habari zinazohusiana na hii