Makala

TAHARIRI: Pesa feki ni hatari kwa uchumi wetu

March 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

TANGU mwaka huu uanze, kumekuwa na ongezeko la visa vya watu kupatikana wakiwa na pesa zinazoshukiwa kuwa bandia.

Mwezi Februari,polisi katika eneo la Ruiru kaunti ya Kiambu, walinasa kwenye nyumba moja pesa bandia za thamani ya Sh32 bilioni.

Pesa hizo zilikuwa mchanganyiko wa Dola, Pauni na za Kenya na zilikuwa. Pesa hizo zilikuwa zimeingizwa kwenye masanduku 20 ya mabati. Tayati washukiwa walifikishwa mahakamani kuhusiana na tukio hilo.

Siku chache baadaye, polisi wamepata pesa nyingine bandia zikiwa zimehiadhiwa kwenye kasha salama ndani ya benki ya Barclays.

Polisi wanasema mteja wa benki hiyo tawi la Queensway jijini Nairobi, aliingiza pesa hizo pia zikiwa za kigeni, zenye thamani ya Sh2 bilioni. Awali polisi wa kitengo cha Flying Squad na wenzao wa kupeleleza Uhalifu (DCI), walikuwa wamekisia kiwango cha pesa kuwa Sh17 bilioni.

Vyovyote iwavyo, pesa hizi ni nyingi mno kuwa zinaweza kuwa mikononi mwa watu. Kusambaa kwa pesa bandia, kunaashiria kuwa humu nchini, kuna watu ambao wana viwanda vya kutengeza fedha hizo, na kuna uwezekano mkubwa kwamba baadhi ya wananchi wanazitumia bila ya kuwa na habari.

Kusambaa kwa pesa nyingi kunatukumbusha mwaka 1992 wakati aliyekuwa kiongozi wa Vijana wa Chama cha Kanu, Bw Cyrus Jirongo, alipokuwa akisambaza pesa kana kwamba alikuwa na kiwanda chake.

Ni wakati huo ambapo noti ya Sh500 ilitolewa kwa mara ya kwanza na hata baadhi ya watu wanaipa jina la Jirongo.

Lakini matokeo yake ni kuwa uchumi wan chi ulisambaratika wakati huo. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1992 ambao Rais Daniel arap Moi alishinda tena, nchi ilijikuta ikipitia kipindi kigumu cha kiuchumi.

Kusambaa kwa pesa bandia wakati huu ambapo Kenya inakumbwa na madeni makubwa, ni hatari kwa uchumi wetu.

Pesa zinaposambaa kwa wingi katika nchi, zinapoteza thamani yake na kufanya kila bidhaa na huduma kuwa ghali. Tukiendelea kuruhusu wahuni wachache wachapishe pesa za ziada na kuzitumia kwenye soko letu, tutakuwa tumeidhinisha kuporomoka kwa uchumi ambao tayari uko katia hali isiyoridhisha.

Polisi wanaochunguza wana wajibu wa kutambua chanzo cha pesa hizo na kukikomesha kabisa. Nchi yetu inahitaji kuimarisha uchumi wake ili wananchi wanufaike kwa jasho lao, na wala si kuruhusu watu wachache watuangamize kwa kutafuta utajiri kwa njia za mkato.