• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
Programu ya simu inayowapunguzia wanawake gharama na kuwaongezea mapato

Programu ya simu inayowapunguzia wanawake gharama na kuwaongezea mapato

Na FAUSTINE NGILA

WAFANYABIASHARA wanawake katika Kaunti ya Nairobi wamekumbatia programu ya kidijitali ili kupunguza gharama na kuongeza mapato.

Akilimali ilimtembelea Bi Juliet Muendi kwenye kibanda chake cha matunda katika eneo la Cabanas na kupata wateja wengi wamemiminika kununua mapapai, maparachichi, ndizi, matikitimaji, matufaha, maembe, machungwa, zabibu na mananasi.

Jua ni kali lakini anamudu kutuelezea jinsi biashara yake imekua polepole hadi ikaweza kujisitiri na sasa anaitegemea kwa kila hitaji la pesa.

“Nilipojitosa katika biashara ya matunda mwaka 2016, nilianza kwa kutumia rukwama kuzungusha bidhaa zangu kutoka eneo moja hadi lingine,” mama huyu mwenye umri wa miaka 34 anasema.

Wakati huo, alikuwa anasafiri kununua matikitimaji, ndizi, mapapai, na maparachichi katika soko la Wakulima, matufaha na zabibu kutoka mtaani Highridge, na kisha kurudi Kitengela kununua maembe na machungwa.

Bi Juliet Muendi kwenye kibanda chake cha matunda katika eneo la Cabanas, Nairobi. Picha/ Faustine Ngila

“Ilikuwa inanigharimu Sh500 kuzunguka katika masoko hayo yote ili kuleta matunda hayo kwa kibanda changu. Lakini mambo yamebadilika sasa,” anasema Juliet, mama wa watoto watatu ambaye kwa sasa hununua matunda yake kutoka kwa programu ya simu Twiga Foods yenye mfumo wa kusambaza bidhaa.

Mfumo wa programu hiyo wa Usimamizi wa Usambazaji (DMS) huwapa soko tayari wakulima ambapo wanunuzi huagiza matunda kupitia kwake kwa bei nafuu.

“Bei ni nafuu ikilinganishwa na kununua kutoka sokoni. Ubora wao wa ndizi unapendwa sana na wateja, kwa sasa ninategemea programu hiyo kununua matunda asilimia 70,” anasema mkazi huyu wa Mlolongo, akiongeza kuwa huduma zinapatikana wakati wowote.

Ameshuhudia ongezeko la mauzo tangu alianza kutumia jukwaa hilo la kidijitali miaka miwili iliyopita, na sasa hategemei tena mshahara wa mumewe kufadhili mahitaji yake kwa kuwa ana faida ya angalau Sh5,000 kwa siku.

Mary Wanjiru, mama mwenye umri wa miaka 28 anafurahi wakati tunapotembelea kibanda chake cha matunda katika mtaa wa Donholm. Anatukaribisha katika biashara yake ambayo imepanuka na sasa anamiliki vibanda vingine viwili.

“Nilipoanza kuuza matunda mwaka 2009, nilikuwa nalazimika kutumia kati ya Sh1,000 na Sh2,000 kwa usafiri nikienda sokoni kusaka matunda. Kila mzigo wa matunda ulipaswa kulipwa,” anakumbuka.

Lakini alipojiunga na jukwaa la kununua la kidijitali la Twiga Foods lilipozinduliwa mwaka 2014, gharama hizo zimepotea na sasa hutumia pesa hizo za ziada kununua matunda zaidi.

Akilinganisha bei kwenye programu hiyo na ile ya soko la Wakulima anaeleza, “Bei za mtandaoni ni nafuu zaidi na zinaleta faida. Kilo moja ya matikitimaji utauziwa kwa Sh30 kwenye programu ikilinganishwa na Sh40 sokoni. ”

Josephine Wanjiku, mwenye umri wa miaka 24, ni mama wa mtoto mmoja mtaani Uthiru anayemiliki duka la kuuza bidhaa za nyumbani.

Alipojitoma kwa biashara mwaka 2017, lengo lilikuwa kumlea mtoto wake bila msaada wowote, na sasa amepata uhuru wa kifedha.

Josephine Wanjiku anasema kuwa bei ya bidhaa kama mafuta ya kupikia, unga na sukari ni nafuu kwa programu hiyo ikilinganishwa na maduka ya kijumla. Hapa ni katika duka lake mtaani Uthiru, Nairobi. Picha/ Faustine Ngila

Awali alitumia akinunua bidhaa zake katika duka la jumla lililo karibu, na alikuwa akilipia hela zaidi kwa bidhaa huku pia akitumia Sh250 kwa usafiri.

Lakini baada ya uvumbuzi huu, sasa anaagiza mafuta ya kupikia, sukari, unga wa ngano na mahindi kupitia kwa programu hii kwa kuwa bei ni nafuu na hakuna usafiri unahitajika. Bidhaa zote huletwa kwa duka lake.

“Nilikuwa nikinunua kilo 10 za sukari kwa Sh2,200, kwa sasa ninazipata kwa Sh2,000. Pakiti 12 za unga wa mahindi huuzwa kwa Sh1150 kwenye maduka ya jumla, lakini kwenye programu hii ni Sh980 tu. Ninapata lita 12 za mafuta ya kupikia kwa Sh1,200 kwenye programu hii zinazouzwa kwa Sh1,400 kwenye maduka ya jumla,” anaelezea.

Kwa sasa jukwaa hili lina watumiaji 18,000, ambapo 11,000 kati yao ni wakulima katika kaunti 20 ambao mazao yao hununuliwa na wateja 7,000 ndani ya Nairobi na maeneo yake.

“Mfumo huu huwafaa wafanyabiashara wa pande zote mbili; wakulima wamehakikishiwa soko tayari kwa mazao yao kwa uwazi, huku wachuuzi wakinufaika na uwepo wa matunda na bidhaa kwa bei nafuu,” anasema Kikonde Mwatela, afisa mkuu wa biashara ya dijitali wa Twiga Foods.

Programu hii hutumia mfumo wa simu ambapo hela za kidijitali hutumika. Mchuuzi huagiza bidhaa kupitia kwa ajenti wa mauzo ambaye hurekodi agizo hilo. Taarifa hiyo hupokelewa na kwa mbashara na oda iliyopigwa kutayarishwa na bidhaa kumfikia mchuuzi siku inayofuata.

Kuundwa kwa programu hii kulichochewa na haja ya kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kama suluhu ya kuwatokomeza mawakala wapunjaji wanaowahangaisha wakulima kwa bei zao duni.

You can share this post!

IG MTEULE: Hillary Nzioki Mutyambai

DOMO KAYA: Jameni tuacheni unafiki!

adminleo