Makala

KOIGARO FALLS: Eneo wazee wa Kalenjin walikuwa wanajirusha kwa kuamini 'kifo kimewasahau'

April 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

NA RICHARD MAOSI

MLIMA wa Koigaro Falls katika eneo la Biribiriet, Kaunti ya Nandi, unasifika kutokana na historia yake ndefu, ya mapango na miinuko ya milima iliyotumika kama makaburi ya wazee wa jamii ya Wakalenjinwaliokatizia maisha yao mle. 

Koigaro itabakia katika kumbukumbu za wengi, na historia kwa kizazi cha kesho kwa kuchangia turadhi za kijamii ingawa haijafikia hadhi ya kuwa makavazi ya kitaifa.

Wazee katika jamii ya Kalenjin kutoka mbali na karibu, walitumia maeneo haya kukatiza maisha yao kwa hiari, bila kulazimishwa na mtu.

Kwa kukosa nguvu za kung’ang’ana maishani wakiwa wanyonge, walikuwa wanajinyima uhai na kukubali kukutana na mauti, ikiaminika wakati wao wa kuondoka duniani ulikuwa umefika.

Inaaminika haya yalitenda kabla ya mienendo ya kikapitalisti inayochangia watu kuuawa kinyama kuingia Kenya. Hapa, kifo kilikuwa ni kwa hiari kwani watu waliishi kwa miaka mingi hadi wakaanza kuamini ‘kifo kimetusahau’. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na tamaduni za jamii ya Nandi, ilikuwa ni kinyume na desturi kwa mtu yeyote kuona kizazi chake cha tatu.

Hivyo, wengi wao waliamua kufuta ‘aibu’ hiyo na kujiua walipojirusha kutoka kwenye majabali ya Biribiriet, ambayo wakazi wanakisia yana kina cha takriban mita 100.

Wakazi wanaamini wengi wao walikuwa wamechoka kusubiri mauti, ikalazimu waungane na mizimu ya babu zao kukwepa mateso ya dunia.

Taifa Leo Dijitali ilipata fursa ya kuzuru mapango hayo, kutangamana na wale waliowahi kushuhudia matukio hayo na kutusimulia historia hiyo yote, ambayo vijana huidhania kuwa ngano.

Hakuna mzee wa kisasa anayeweza kukubali kujirusha mle. Panatisha! Picha/ Richard Maosi

Koigaro inapatikana Kusini mwa Kaunti ya Uasin Gishu, zaidi ya kilomita 20 kutoka mjini Eldoret kupakana na mji wa Kapsabet.

Ardhi hapa ni yenye rutuba ya kutosha, wakazi wengi wakitegemea kilimo na ufugaji wa ng’ombe kwa maisha yao.

Mwelekezi wetu Elkanah Kipkemboi Tenai alitufikisha kwenye maporomoko ya maji yaliyotukaribisha katika mapango na mlima wa Koigaro.

Kabla ya kuja kwa wakoloni, Koigaro ilikuwa makao ya wanyama mwitu kama vile chui, fisi, simba, mbwa mwitu na nyoka.

Kina cha bonde hili kinatisha. Wazo la kujirusha labda lichochewe na uendawazimu. Picha/ Richard Maosi

Inasemekana wanyama hawa walikuwa wamebadilisha sehemu hii kuwa hifadhi ya kudumu, kwani walipata lishe ya kutosha kutokana na mizoga ya wazee wakongwe waliokuwa wakijirusha.

Bi Taprendich Kogo mwenye zaidi ya miaka 112 anasema alizaliwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Kipindi hicho, alikuwa msichana mdogo na alielewa fika mambo yote yaliyokuwa yakitendeka Koigaro Falls, kwa kutazama na kusikia.

Anasema kwamba mumewe alizaliwa kati ya 1908-1910, wakoloni wakianza kutua Afrika Mashariki.

Bi Taprendich Kogo alituhadithia yote aliyoshuhudia wakati akiwa msichana. Picha/ Richard Maosi

Alikuwa msichana wa miaka 18 ilipotimu 1935, akisema alikuwa anaishi Biribiriet na wazazi wake, akiwasaidia kulisha mifugo na kukuza mimea.

Anaeleza kuwa chui, simba na nyoka walikuwa wakitembea na kuishi katika kijiji chao, bila kudhuru binadamu na baadaye kurudi kwenye mapango yao kusaka masalio ya mizoga.

Kogo hakubahatika kuwa na watoto wengi, isipokuwa binti mmoja, kwani alikuwa akitembea kila sehemu kutafuta mizizi ya madawa ya kienyeji.

“Katika ujana wangu nilipata mume nikiwa nimechelewa kwa sababu nilikuwa tabibu wa madawa ya kienyeji, nilitumia wakati mwingi kudadisi aina ya mitishamba,” anasema.

Sehemu ya chini ya bonde la Koigaro. Hapa ungewapata fisi, chui na sima wakisubiri wazee hao kujirusha. Picha/ Richard Maosi

Kazi yake ilimfanya ajifundishe lugha nyingi, maana alifanya kazi kwa ushirikiano na watu wa makabila tofauti katika takriban kila pembe ya nchi hii.

Alijaliwa kupata binti mmoja tu anayefahamika kama Grace Kogo mnamo 1952.

Taprendich anasema wazee walikuwa wakiitana kutoka vijiji vya Kipkorian, Biribiriet, Lelmokwo na Koigaro wakajikusanya na kufikisha idadi iliyokuwa ikihitajika kujiua.

Hatimaye walishikana mikono na kuelekezana hadi kwenye mlima wa Koigaro huku wakiimba nyimbo.

Kogo alituimbia nyimbo hizo japo kwa lugha ya Kinandi na mfasiri wetu akatuelezea wimbo ulikuwa ukiwapatia motisha wasije wakaogopa. Wafahamu kuwa walikuwa pamoja katika zoezi zima.

Ilikuwa lazima wazee hao kukusanyika na kufikisha idadi iliyokuwa ikihitajika kujiua. Picha/ Richard Maosi

Alisema kuwa kinyume na wanaume wa kisasa, wazee wa zamani walikuwa hawasilikilizi mawaidha ya wake zao wala kubembelezeka na labda ndio sababu ilikuwa vigumu kuwazuia.

“Kando na jamaa zao kuwazuia kushindikana, pia tabia hii ilibadilika na kuwa desturi ya watu wetu,” alisema.

Familia zao hazikuwa na uwezo wa kuwazuia, muradi tu walikuwa wameamua, ilibidi maaamuzi yao kuheshimiwa na jamii.

“Walikuwa wanasimama kwenye majabali huku wameshikana mikono na kuimba nyimbo za kuwapa hamasa kabla ya kujirusha kinyumenyume,” anaeleza.

Elkana alituonyesha njia ambayo wazee hao walikuwa wanapitia wakati wakienda kujiua. Picha/ Richard Maosi

Walipotua ndani ya mapango wanyama mwitu walikuwa tayari kuwatafuna na kugawana sehemu zao za mwili.

Kwa bahati mbaya aliyechukua muda mrefu ndani ya pango bila kuliwa na wanyama mwitu, wazee wa kijiji walichinja mbuzi, na mzoga wake ukatumika kuwatakasa kama njia ya kuondoa laana katika jamii.

Lakini Kogo anaamini kuwa mzoga ulikuwa uwavutie wanyama waliokuwa wameshindwa kuupata mwili wa mhusika.

“Kati ya mwaka wa 1960-90, kulikuwa na mifupa ya watu hapa, lakini ilisombwa na maji. Ile iliyosalia ilikusanywa na wanakijiji kisha wakaiteketeza,” anasema.

Simion Arap Rotich Sitama, 90, ni jirani yake na alikuwa mzee wa mtaa kwa miaka 39 katika eneo la Lelmokwo na Biririet.

Anakubaliana na kauli ya Bi Kogo kuwa wazee hawakustahili kuona kizazi cha tatu kwa mujibu wa tamaduni zao.

Simion Arap Rotich Sitama wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali. Picha/ Richard Maosi

Anasema alisikia ripoti kutoka kwa baba yake kuwa wazee walikuwa wakijirusha hasa wale wa ukoo wake wa Kimnyinget.

Hata wakati mmoja baba yake alitaka kujirusha lakini alizuiliwa na wazee wa kijiji, kwa sababu usasa ulikuwa umeanza kuingia na watu walishaanza kuona mwanga.

“Miaka ya sitini kabla ya uhuru, baadhi ya familia bado zilikuwa zikiendesha tamaduni hii ijapokuwa kisiri,” alisema.

Alieleza kuwa watu wengi walikuwa wameanza kupata mwanga na kuachana na tamaduni yenyewe ijapo shingo upande.

Dini na elimu ni miongoni mwa mambo yaliyosaidia kwa asilimia kubwa kupambana na kasumba ya wazee kujitoa uhai.

Elkana akichungulia kina cha bonde hilo ambapo urefu wake ni takriban mita 100. Picha/ Richard Maosi

Anasema wazee wengi walikuwa wakisema wanataka kukatiza maisha yao kutokana na mahangaiko ya wabeberu na uzee.

Walidanganya familia zao kuwa wamekwenda safari ya mbali na wangerejea lakini hawakurudi.

“Wengi wao walitoa madai kwamba hawakuwa na nguvu za kufanya kazi na hivyo basi hawakuona haja ya kuendelea kuishi,” akasema.

Siku hizi eneo la Koigaro linatumika na wanakijiji kuendeshea shughuli zao za kawaida kama vile kunyunyizia mimea maji na kufua nguo.

Vilevile wapendanao humiminika hapa, kuvinjari mandhari kwa sababu ni eneo tulivu na lenye taswira ya kuvutia.

Maji ya Koigaro sasa hutumika kunyunyizia mashamba maji. Picha/ Richard Maosi

Bali na uzuri wake wote, ni eneo hatari kwa usalama, hasa msimu wa mvua ambapo wageni wengi wametoweka kwa kuzama majini na hatimaye kumezwa na mabonde wasipatikane.

Elkana anasema huenda ni nguvu za wazee ambazo zimekuwa zikiwavuta wanapokuja kuzuru maeneo haya.

“Wakati mwingine utasikia sauti za watu wakizungumza na kucheka,” anaongezea.

“Mitaa ya Langas, Kapseret, Mlango na Lelmokwo imewapoteza watu wengi katika sehemu hii wasipatikane kwa sababu ya utelezi unaosababishwa na maji mengi msimu wa mvua,” anasema.

Anaomba serikali kuorodhesha Koigaro miongoni mwa makavazi ya kitaifa, akiamini itasaidia kuwapatia vijana ajira.

“Wengi wao wanaelewa historia ya babu zao, pia wanaweza kujiajiri kuwaelekeza watalii, na nafasi hizi za kazi zitachangia pato la kitaifa.”