Habari Mseto

Madereva Lamu wapinga ada ya vizuizi kuongezwa

March 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA KALUME KAZUNGU

MADEREVA na utingo wa mabasi ya usafiri wa umma yanayotumia barabara ya Lamu kuekelea Mombasa wameilalamikia serikali ya kaunti ya Tana River kwa kuongeza ada ya kuvuka kizuizi cha polisi eneo la Minjila kutoka Sh 100 hadi Sh 300.

Wakizungumza katika eneo la Mokowe Jumatano,  madereva hao walitisha kususia kazi iwapo serikali ya kaunti hiyo itaendelea kuwakandamiza kwa kuwaitisha ada hiyo waliyoitaja kuwa ya juu.

Mnamo Jumatano, abiria zaidi ya 200 walilazimika kukaa eneo hilo la Minjila kwa zaidi ya saa tatu kutoka saa saba unusu mchana hadi saa kumi jioni baada ya madereva na utingo wa mabasi sita kudinda kulipa ada hiyo mpya.

Baadhi ya abiria na mabasi yaliyozuiliwa katika kivuko cha Minjila baada ya madereva kudinda kulipa ada mpya iliyopandishwa kutoka Sh100 hadi Sh300 mnamo Februari 28, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Mabasi hayo yaliyokuwa yakielekea Mombasa ilhali mengine yakielekea Lamu yalizuiliwa na askari wa kaunti kwa ushirikiano na polisi wa utawala wanaoshika doria kwenye kizuizi hicho cha Minjila.

Iliwalazimu abiria kutoa fedha zao za mfukoni ili kuruhusiwa kuendelea na safari zao.

Bw Salim Hassan, ambaye ni dereva wa basi la kampuni ya Mombasa Raha alisema hawako tayari kulipa ada hiyo hadi pale watakapofafanuliwa sababu iliyopelekea kodi hiyo kupandishwa kutoka Sh 100 hadi Sh 300.

Bw Hassan pia aliitaka kaunti kuwaeleza wasimamizi wa kampuni zinazomiliki mabasi hayo badala ya kuwashurutisha madereva kulipa fedha hizo.

Baadhi ya mabasi yaliyozuiliwa katika kivuko cha Minjila baada ya madereva kudinda kulipa ada mpya iliyopandishwa kutoka Sh100 hadi Sh300 mnamo Februari 28, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

“Kampuni zetu hazijafahamishwa kuhusu mabadiliko hayo ilhali wao wanatushurutisha sisi madereva kutoa fedha hizo. Kampuni zetu zijulishwe kwanza,” akasema Bw Hassan.

Naye Bw Basheikh Yusuf wa basi la T.S.S alieleza kutoridhishwa kwake na mageuzi hayo ya ghafla ambayo alisema huenda yakaathiri pakubwa biashara yao.

“Ikiwa kila basi litakalopita kwenye kivuko hicho linatoa Sh 300, hii inamaanisha hakuna faida yoyote tutapata. Ada hiyo ni ya juu mno na tunataka waache tuendelee kulipa Sh 100,” akasema Bw Basheikh.