• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Serikali yaelekeza macho Amerika kusaka wafadhili

Serikali yaelekeza macho Amerika kusaka wafadhili

Na VALENTINE OBARA

MASUALA kuhusu ustawi wa kiuchumi, uwekezaji na vita dhidi ya ufisadi yanatazamiwa kupewa kipaumbele maafisa wakuu wa Serikali ya Kenya watakapokutana na wenzao wa Amerika jijini Washington.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Bi Monica Juma ataongoza ujumbe wa serikali katika ziara hiyo nchini Amerika kuanzia Jumanne hadi Jumatano.

Wizara hiyo ilisema, miongoni mwa watakaoandamana na Bi Juma ni maafisa wa ngazi za juu serikalini.

Masuala ambayo yanalengwa kujadiliwa wakati wa ziara hiyo itakayohusisha mikutano na maafisa wa serikali ya Amerika ni kuhusu ushirikiano wa biashara na kiuchumi, masuala ya ulinzi, demokrasia na uongozi na yale yanayohusu ukanda huu.

“Katika ukuzaji wa uchumi, biashara na uwekezaji, Kenya na Amerika zinalenga kustawisha ushirikiano ambao utakuza uchumi kwa kuleta nafasi zaidi za ajira na uwezo wa kiufundi,” wizara hiyo ikasema kwenye taarifa kwa wanahabari.

Kenya pia inatazamia kutafuta ushirikiano mkubwa zaidi utakaoboresha biashara zinazoendelezwa chini ya Sheria ya AGOA inayotoa nafasi za ustawi wa kibiashara Afrika.

Katika masuala ya ulinzi, serikali inanuia kutafuta ushirikiano zaidi wa kuimarisha uwezo wa kijeshi ili kukabiliana na changamoto za kiusalama humu nchini na katika mataifa ya ukanda huu. Pia inatarajiwa kuwepo kwa mashauriano kuhusu mbinu za kukuza demokrasia na uongozi bora nchini.

“Kenya na Amerika zitajadiliana kuhusu masuala yanayohusu mataifa hayo mawili, ikiwemo maadili ya kidemokrasia, juhudi za kupambana na ufisadi na jinsi ya kushirikisha raia katika uboreshaji wa usalama kitaifa,” ikasema wizara hiyo.

Mkutano huo utafanyika siku chache tu baada ya Bi Juma kukutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza ambaye alizuru Kenya wiki iliyopita.

Wiki chache zilizopita, ziara iliyofanywa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga nchini Uchina, iliripotiwa kuambulia patupu katika harakati za kutafuta ufadhili wa ujenzi wa reli kisasa, SGR, kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Ingawa hali hiyo ilionyesha ishara mbaya ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Kenya na Uchina ambao umekuwepo tangu Rais Kenyatta alipoingia mamlakani 2013, serikali ilikanusha kwamba suala la ufadhili wa SGR lilijadiliwa wakati wa ziara hiyo.

Mkutano huo wa Bi Juma nchini Amerika unatokea pia siku chache baada ya Rais Kenyatta kufanya mabadiliko katika wizara hiyo kwa kubadilisha mabalozi mbalimbali akiwemo yule wa Kenya nchini Amerika.

Mnamo Ijumaa, serikali ilitangaza Bw Robinson Githae ambaye amekuwa balozi wa Kenya nchini Amerika, kuwa balozi mpya nchini Austria kuchukua mahali pa aliyekuwa Waziri wa Michezo, Hassan Wario ambaye amesimamishwa kazi.

Balozi mpya wa Kenya nchini Amerika sasa atakuwa Bw Lazarus Amayo, ambaye kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York.

Vile vile, aliyekuwa Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Bw Michael Mubea aliteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Dublin.

Akiidhinishwa, Bw Mubea atachukua mahali pa Bw Richard Opembe ambaye amehamishwa hadi Madrid kuchukua mahali pa Severine Luyali.

You can share this post!

Jina langu si tiketi ya Ikulu, Ruto aambia wapinzani

Wabunge wahimizwa kuinua maisha ya vijana wenzao

adminleo