Tanzania kujitoa katika mpango wa UN kuwapa wakimbizi uraia
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Na AFP
Kwa Muhtasari:
- Tanzania ilijiondoa kutokana na ukosefu wa fedha na utovu wa usalama
- Nchi hiyo imekuwa ikiwahifadhi raia kutoka Burundi na DRC
- Kulingana na UNHCR, wakimbizi wanafaa kupewa uraia wa nchi wanazokimbilia hifadhi
RAIS wa Tanzania, John Magufuli, ametangaza kuwa nchi yake itajiondoa kutoka mpango wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia wakimbizi ambao unatoa suluhisho la kudumu kwa wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuwapa uraia.
“Tanzania imeamua kujiondoa kwa sababu za usalama na ukosefu wa fedha,” ilisema taarifa ya serikali.
Rais Magufuli alitoa tangazo hilo Ijumaa katika mkutano na mabalozi wa nchi za kigeni jijini Dar es Salaam.
Mnamo Januari, Tanzania ilifahamisha shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), kuwa ilisimamisha kuwapa uraia baadhi ya wakimbizi kutoka Burundi na kuwa isingekubali maombi mapya kutoka kwa wakimbizi.
Nchi hiyo imekuwa ikiwahifadhi raia kutoka Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.
Kulingana na gazeti la serikali la Tanzania Daily News, Magufuli analaumu jamii ya kimataifa kwa kukataa kuipatia pesa ilizoahidi kusaidia wakimbizi.
Kulingana na UNHCR, wakimbizi wanafaa kupatiwa uraia wa nchi wanazokimbilia hifadhi.
Shirika hilo linaamini kwamba wakimbizi wakipatiwa elimu na haki ya kufanya kazi kisheria, wanaweza kupata maarifa na kujitengemea huku wakichangia katika uchumi wa nchi wanazoishi.