• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
OBARA: Ni aibu Kenya kuendelea kutegemea mvua pekee

OBARA: Ni aibu Kenya kuendelea kutegemea mvua pekee

Mradi mkubwa wa kunyunyiza maji katika shamba la Galana-Kulalu haueleweki unakoelekea, na wala haijulikani serikali ina makubaliano gani na kampuni zinazoutekeleza. Picha/ Maktaba

Na VALENTINE OBARA

MWISHONI mwa wiki iliyopita, kulikuwa na shangwe katika pembe tofauti za nchi wakati mvua kubwa iliponyesha baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kilichoshuhudiwa tangu mwaka uliopita.

Licha ya kuwa idara ya utabiri wa hali ya hewa ilieleza wazi kwamba mvua hii ni ya muda mchache, wananchi wengi walionekana kuwa na matumaini kwamba hatimaye kutakuwa na afueni katika uzalishaji wa chakula na ongezeko la kiwango cha maji, hali ambayo itasaidia kuwapunguzia gharama ya maisha.

Hakika, utabiri kamili wa hali ya hewa ni kuwa msimu wa mvua ambao hutarajiwa kuanza Machi utachelewa hadi mwisho wa mwezi au mwanzoni mwa Aprili na mvua yenyewe itakuwa ya kiwango kidogo.

Shangwe zilizoshuhudiwa, sio tu kutoka kwa wananchi bali pia katika vyombo kadhaa vya habari, ni ishara tosha kwamba masaibu yanayotukumba kuhusiana na gharama kubwa ya mahitaji yetu muhimu yanatokana na uzembe wetu wa kutotilia maanani mbinu za kisasa za uzalishaji na uhifadhi wa chakula na maji.

Katika karne hii ni aibu kuwa taifa la Kenya lenye hadhi kubwa barani Afrika bado linategemea mvua kwa kilimo chake.

 

Teknolojia

Kilimo kingali mojawapo ya sekta kuu zinazochangia zaidi kwa uchumi wa taifa na hivyo basi ingekuwa busara kama katika enzi hii tungekuwa tunatumia teknolojia za kisasa kwa uzalishaji wa chakula bila kutegemea mvua jinsi tunavyofanya.

Kuna mataifa mengi ambayo ni majangwa ilhali yanafanikiwa kuzalisha chakula kwa wananchi wao. Humu nchini tumebarikiwa na rotuba bora lakini changamoto kuu ni maji ya kutosha, na hili ni changamoto linaloweza kusuluhishwa kwa kuwekeza kwa miradi ya kunyunyiza maji mashambani.

Tunajua unyunyizaji ni miongoni mwa mipango mikuu ya serikali ya Jubilee, lakini kuna jambo muhimu linalofaa kueleweka. Katika nchi hii, tegemeo kubwa zaidi kwa uzalishaji wa chakula kinachotumiwa na wananchi ni wakulima wadogo.

Ikiwa serikali inanuia kutumia unyunyizaji maji mashambani kuongeza kiwango cha chakula ili kutosheleza mahitaji ya wananchi, ni wakulima hao wadogo ambao wanapaswa kuwezeshwa kuwekeza katika unyunyizaji ka mashamba yao.

 

Mradi haueleweki

Ilivyo kwa sasa, mradi mkubwa wa kunyunyiza maji katika shamba la Galana-Kulalu haueleweki unakoelekea, na wala haijulikani serikali ina makubaliano gani na kampuni zinazoutekeleza. Hivyo basi kuzungumzia matumaini yake kuleta afueni kwa wananchi itakuwa ni kubahatisha tu.

Mbali na hayo, kuna maeneo ya nchi hii ambayo huwa hayafahamu njaa kwa kuwa chakula kingi huzalishwa mwaka mzima.

Kama tungekuwa na nia ya kuondolea taifa janga la njaa linaloshuhudiwa maeneo tofauti kila mwaka, maeneo hayo yenye vyakula vingi yangepewa vyombo vya kisasa vya kuhifadhi vyakula ili visafirishwe hadi maeneo yenye mahitaji.

Serikali za kaunti pia ziwe katika mstari wa mbele kuleta mabadiliko haya badala ya kuachia serikali kuu na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu mzigo mzima wa kuokoa wananchi kutokana na njaa.

 

You can share this post!

TAHARIRI: Kwa nini kila msimu mvua ilete maafa?

WASONGA: Naam vyuo vya kiufundi visibadilishwe kuwa vyuo...

adminleo