Habari Mseto

Uzani mdogo wafanya vijana kukataliwa jeshi

February 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Shughuli ya vijana kusajiliwa kwenye kikosi cha jeshi la Kenya (KDF) kaunti ya Lamu ikiendelea Februari 12, 2018. Vijana wengi walitemwa kwa kukosa kufikisha uzani unaohitajika. Picha/ Kalume Kazungu

KALUME KAZUNGU na FADHILI  FREDRICK

MAKURUTU wengi waliojitokeza kutafuta nafasi ya kusajiliwa kwenye kikosi cha jeshi la Kenya (KDF) kaunti ya Lamu Jumanne walitemwa kutokana na kupungukiwa na uzani wa mwili uliohitajika.

Zaidi ya makurutu 30 hawakuweza kufikisha kilo 54.5 kwa upande wa wanaume na kilo 50.0 kwa upande wa wanawake kama ilivyohitajika.

Wengi wa makurutu waliojitokeza kwa shughuli hiyo iliyofanyika katika bustani ya Kibaki mjini Lamu walikuwa na uzani wa kati ya kilo 49 kwenda chini.

Afisa Msimamizi wa shughuli ya usajili wa makurutu kuingia jeshini katika kaunti ya Lamu, Luteni Kanali Zacharia Burudi, aliambia wanahabari kuwa idadi kubwa ya makurutu pia walitemwa nje kutokana na meno yaliyobadilishwa rangi kufuatia ulaji mwingi wa miraa.

Bw Burudi kadhalika alisema kiwango duni cha masomo hasa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne (KCSE) pia ni kizingiti kilichopelekea vijana wengi wa Lamu kukosa nafasi ya kusajiliwa kujiunga na KDF.

Aliwasihi wazazi na utawala wa kaunti ya Lamu kutoa hamasa kwa vijana wajiepusha na ulaji mwingi wa miraa unaoharibu meno yao.

Pia aliwahimiza wakazi wa Lamu kujikaza zaidi kimasomo ili wafaulu kuajiriwa serikalini, ikiwemo kupata nafasi za ajira jeshini.

 

Kilo 49

“Wanaume wanahitajika kuwa na kilo 54.5 ilhali wanawake wanastahili kuwa na kilo 50.0. Wengi wao tuliwatoa mapema kwani walikuwa na uzani wa kilo 49 kwenda chini” akasema Bw Burudi.

Katika kaunti ya Kwale, zaidi ya wanawake 30 walijitokeza eneobunge la Msambweni, lakini wakafahamishwa kuwa KDF ilitaka wanaume pekee.

Wanawake waliokuwa wamejitokeza kushiriki zoezi hilo lililofanyika katika Shule ya Msingi ya Jomo Kenyatta walikasirishwa na hatua hiyo na kusema kuwa sio mara ya kwanza kuondolewa kwa sababu ya jinsia.

“Mwaka 2017 walitoa udhuru kama huo. Je, inamaanisha hakuna nafasi zaidi kwa wanawake katika jeshi?” mwanamke mmoja aliuliza, akiongeza kuwa hii ni mara ya pili wanawake kuondolewa katika zoezi hilo.