Habari MsetoSiasa

Kalonzo ajipata kwa njiapanda: Je, niapishwe? Niondoke NASA? Vipi 2022? Wakamba watanifuata?

February 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Kinara wa NASA na kiongozi wa chama cha Wiper Bw Stephen Kalonzo Musyoka. Maswali manne kuhusu siasa yanamkosesha usingizi. Picha/ Maktaba

Na WYCLIFFE MUIA

Kwa Muhtasari:

  • Bw Musyoka amejipata kona mbaya ya kisiasa kutokana na shinikizo za kuapishwa
  • Wiper inaangazia zaidi kinyang’anyiro cha urais 2022, kitapuuza chochote kinachoweza kuzuia Bw Musyoka kuwania urais
  • Bw Musyoka atishia kujiondoa NASA iwapo baadhi ya viongozi wa NASA wataendelea kumtusi
  • Anakabiliwa na hatari ya kutengwa na baadhi ya wafuasi wa upinzani kwa ‘kuwasaliti’ kuhusu suala la kiapo
  • Huenda Mudavadi, Kalonzo na Wetang’ula wakaungana na kuanza kutafuta kura za Mlima Kenya

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka Jumanne alikiri kuwa suala la kula kiapo kama ‘naibu rais wa wananchi’ linamnyima usingizi huku akikiri kuwa hatua hiyo itakuwa kinyume cha sheria.

Makamu huyo wa zamani wa Rais amejipata kona mbaya ya kisiasa kutokana na shinikizo za kuapishwa kama ‘naibu rais wa wananchi’ huku washauri wake wakuu wakimuonya kuwa huenda hatua hiyo ikaathiri azma yake ya urais ifikapo 2022.

Wakili Kioko Kilukumi anasema iwapo Bw Musyoka atashtakiwa kwa kula kiapo na apatikane na hatia, huenda akazuiliwa kisheria kuwania urais, suala ambalo Wiper ingetaka kuzuia.

Akiongea na wanahabari Jumanne, Bw Musyoka alikanusha ripoti kuwa ataapishwa Februari 28 na kusisitiza kuwa anaendelea kushauriana kwa kina na vinara wenza wa upinzani kabla ya kutangaza msimamo wake kamili.

 

Anaangazia 2022

Mwenyekiti wa chama cha Wiper ambaye pia ni Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana alisema chama hicho kinaangazia zaidi kinyang’anyiro cha urais 2022, na kuwa kitapuuza chochote kinachoweza kuzuia Bw Musyoka kuwania urais wakati huo ukifika.

Tangu kinara wa NASA Raila Odinga aapishwe Januari 30, Bw Musyoka amekuwa akikejeliwa na baadhi ya viongozi na wafuasi wa upinzani kwa madai kuwa ni “mwoga” huku wengine wakitaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho achukue nafasi yake katika NASA.

Jumanne, Bw Musyoka alitishia kujiondoa NASA iwapo baadhi ya viongozi wa NASA wataendelea kumtusi kuhusiana na hatua yake ya kususia kiapo.

 

Kutumiwa na Jubilee

“Mimi na Raila ni kama pacha na sielewi kwa nini viongozi wachache ndani ya NASA wanatumiwa na Jubilee kuleta mgawanyiko. Nawaonya viongozi hao kuwa tuna uwezo wa kujiondoa katika muungano tuone watafanya nini,” alisema Bw Musyoka.

Alisema kuwa atakutana na vinara wenzake wa NASA: Bw Odinga (ODM), Musalia Mudavadi (Amani National Congress) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) ili kujadili kwa kina suala la kiapo chake.

“Raila mwenyewe na mimi Kalonzo tunajua vyema kuwa kiapo hiki ni kinyume cha Katiba. Huo ndio ukweli wa mambo. Iwapo tutakubaliana kuwa tutakula kiapo kinyume cha Katiba na tuelewane jinsi ya kukabiliana na athari zake ni sawa.

Mimi niko tayari wakati wowote kuapishwa,” alisema Bw Musyoka jana baada ya kufanya kikao na kundi la viongozi wanawake wa chama cha Wiper mjini Athi River.

 

Hatari ya kutengwa

Kwa upande mwingine, Bw Musyoka anakabiliwa na hatari ya kutengwa na baadhi ya wafuasi wa upinzani na kutemwa kwa ‘kuwasaliti’ kuhusu suala hilo la kiapo. Pia kuna suala la iwapo ngome yake ya Ukambani itamfuata akiamua kujiondoa NASA.

Jumamosi iliyopita, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama alitishia kumgonga Bw Musyoka na Biblia kichwani iwapo atasita kuapishwa.

Naye naibu kinara wa Wiper Farah Maalim aliweka wazi kuwa hakuna uwezekano wa Bw Musyoka kula kiapo kama ‘naibu rais wa wananchi’. “Sidhani kuwa Kalonzo ataapishwa. Ningefurahia sana iwapo Kalonzo angechukua msimamo imara na kusema, ‘samahani mimi ni wakili sitaki kufanya haya’,” alinukuliwa Bw Maalim.

Naibu Spika huyo wa zamani alidai kuwa Bw Odinga ndiye alishinikiza ulaji wa kiapo, uamuzi ambao ulipingwa na vinara wenzake watatu.

 

Mpasuko ndani ya NASA

“Tangu mwanzo Kalonzo, Wetang’ula na Mudavadai walipinga vikali kuapishwa. Sioni NASA ikidumu baada ya kiapo cha Raila. Natabiri kuwa Mudavadi, Kalonzo na Wetang’ula wataungana na kuanza kutafuta kura za Mlima Kenya. Siasa ndio zimeanza,” aliongeza Bw Maalim.

Madai ya Bw Maalim hata hivyo yalikanushwa na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr, akisema hayo ni maoni yake kibinafsi na wala sio ya chama cha Wiper.

Viongozi wa Wiper wamekuwa wakisisitiza kuwa wanajiandaa kuzindua mikakati ya kumtawaza Bw Musyoka kuwa mwaniaji wa urais 2022.

Prof Kibwana alisisitiza kuwa mkataba wa maelewano baina ya vigogo wa NASA ni sharti ufuatwe na Bw Odinga hafai kuwania tena urais 2022.

Gavana Kibwana alisema wakati umewadia kwa Bw Odinga kurudisha shukrani kwa kuunga mkono Bw Kalonzo katika kinyang’anyiro cha urais 2022.