Habari MsetoKimataifa

Mkenya matatani kwa kuwaua wanawake 11 Amerika

May 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MKENYA anayeishi Marekani amefunguliwa mashtaka ya kuwauwa wanawake 11 wakongwe na kuiba mali ya thamani kubwa, eneo la Dallas, Texas.

Billy Chemirmir mwenye umri wa miaka 46 alikamatwa kufuatia mauaji ya mwanamke wa miaka 81, na Jumanne Mei 21 akafunguliwa mashtaka sita, kuhusu mauaji ya wanawake wa kati ya miaka 76 na 94.

Kulingana na mashirika ya habari nchini Marekani, Chemirmir amekuwa kuzuizini kutoka Machi 2018 kuhusiana na mauaji ya Lu Thi Harris, 81, ambaye alikuwa mkazi wa Dallas.

Polisi wanadaiwa kupata ushahidi uliomhusisha na mauaji ya Harris, wakati alipokuwa akihojiwa kuhusiana na mauaji hayo na mtu asiyeaminika akampigia simu.

Mwanamume huyo aidha anadaiwa kuwa alivunja na kuingia katika nyumba ya ajuza wa miaka 91 Machi 2018 na kusababisha mauaji, ambacho kilikuwa kiini cha kukamatwa kwake.

Mashirika ya habari yaliripoti kuwa mwanamume huyo alimpiga ajuza huyo kwa pilo hadi akapoteza fahamu, kisha akaiba mali yake. Wahudumu wa afya walipofika na kumuamsha, ajuza huyo anaripotiwa kuwaambia kuwa mvamizi ndiye aliyepora mali yake.

Polisi walichunguza na kubaini kuwa Chemirmir ndiye alikuwa mvamizi huyo, kisha wakampata na mali hizo, zikiwa ndani ya sanduku ambalo aidha lilikuwa limeibiwa kwa Harris.

Polisi wanadai mshukiwa alikuwa akitumia ujuzi wake katika utoaji wa huduma za afya kuwadhulumu wazee, ambao ni viumbe dhaifu katika jamii.

Polisi sasa wanachunguza visa vya mauaji ya maajuza 750, ambavyo havijawahi kutatuliwa, kuona ikiwa kuna uhusiano wowote.

Wakili wake, hata hivyo, alisema kuwa hawajui mahali mashtaka hayo yalitolewa, kando na lile la Harris ambalo lilifanya akamatwe.