ULAFI: Wabunge watisha kuteka nchi wakipigania matumbo yao
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE na maseneta Alhamisi waliitaka Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu (SRC) ikubali waendelee kulipwa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi la sivyo wakatae kupitisha bajeti ya mwaka huu.
Waliamua kupambana mahakamani hadi amri iliyotolewa wiki jana ya kuzima malipo hayo itupiliwe mbali.
Walisema ni haki yao kisheria na kikatiba kulipwa pesa hizo sawa na maafisa wengine wakuu serikalini, wakiongeza kuwa SRC inafaa kuondoa kesi iliyowasilisha mahakamani kuzima malipo hayo.
Wabunge ambao tulizungumza nao baada ya mkutano wao wa faragha Alhamisi, walisema kuwa tayari fedha za kugharamia malipo ya marupurupu hayo zimetengwa kwenye bajeti ya Tume ya Huduma za Bunge (PSC) mwaka huu.
Mkutano huo, usio rasmi, uliongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka.
“Marupurupu yetu ya nyumba tayari yamejumuishwa katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 ambao unaanza Julai 1, 2019. Kwa hivyo, malipo hayo hayataathiri mipango ya serikali kwa njia yoyote,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake kwa sababu walikubaliana katika “kamukunji” hiyo kutofahamisha wanahabari mambo waliyojadili.
Asasi ya bunge imetengewa Sh36.6 bilioni katika bajeti ijayo ambayo itasomwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich kabla ya tarehe 20, mwezi huu.
“Ikiwa maafisa wa serikali kama vile mawaziri na makatibu wa wizara hupokea marupurupu ya nyumba, mbona sisi tunyimwe? Tumeamua kwa kauli moja kwamba PSC itaendelea kutulipa pesa hizo licha ya kesi inayoendelea mahakamani,” akasema.
Wiki jana, mahakama kuu iliiagiza tume ya PSC kutoendelea kuwalipa wabunge na maseneta 416 marupurupu hayo hadi kesi iliyowasilishwa na SRC itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Vilevile, SRC chini ya mwenyekiti wake Bi Lyn Mengich inaitaka mahakama kuu kuamuru kwamba wabunge hao warejeshe fedha ambazo tayari wamelipwa kama marupurupu ya nyumba kwani hatua hiyo ni kinyume cha sheria.
Tume hiyo inashikilia kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kukadiria na kuidhinisha mishahara na marupurupu yote ya maafisa wa serikali, wakiwemo wabunge.
Mwanaharakati Okiya Omtata Okoiti pia amewasilisha kesi mahakamani kupinga malipo hayo.
Katika kesi yake, Bw Omtata amewashtaki wabunge na maseneta wote 416 kama watu binafsi.
Katika mkutano wa jana, wabunge na maseneta walikubaliana kuwa kesi hizo mbili ziwekwe pamoja na iwe kesi moja ambapo mshtakiwa ni tume ya PSC wala sio wao kama watu binafsi.
“Vilevile, tumekubaliana kuwa PSC ndiyo iwe ikisimamia masuala yote ya mishahara na marupurupu yetu kwa sababu hii ni tume ya kikatiba ilivyo SRC,” akasema mbunge mmoja.
Baada ya mkutano huo, uliodumu kwa saa mbili kwenye ukumbi wa bunge, wabunge waliondoka wakiwa na furaha huku wakikataa kuongea na wanahabari waziwazi.
“Leo (jana) hatuongei na nyinyi. Haya ni masuala mazito yanayohusu sisi peke yetu,” akasema Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale, baada ya kikao hicho.