Lazima TSC itekeleze amri ya mahakama – KNUT
Na VITALIS KIMUTAI
WALIMU kupitia muungano wa KNUT wameitisha mkutano na Tume ya Kuwaajiri (TSC) Jumatatu ili kujadili sulala la utekelezaji wa amri iliyotolewa na korti kuhusu kupandishwa madaraka la sivyo watagoma.
Walimu hao wamesema kuwa sharti tume ya TSC itekeleze amri hiyo ambayo ilitolewa na Mahakama ya Kusuluhisha Mizozo baina ya Waajiri na Waajiriwa.
Aidha, Katibu Mkuu wa Knut Wilson Sossion alisema endapo TSC itakata rufaa ya uamuzi huo wa Jaji Bryam Ongaya, basi walimu watagoma.
Katika kesi hiyo ambayo Knut iliwasilisha kortini mnamo Januari 2 mwaka huu kuhusu masuala kadha ambayo walimu wamekuwa wakitofautiana na mwajiri wao, TSC ilipoteza.
Hata hivyo, Knut imesema kuwa iko tayari kuketi na TSC kujadili jinsi ya kutekeleza amri ya korti.
“Knut iko tayari kuketi na TSC na kujadili jinsi ya kutekeleza kikamilifu amri za korti kuhusu jinsi ya kupandisha walimu madaraka, kurejesha maafisa wa muungano ambao walihamishiwa shule za mbali na maeneo yao ya uwakilishi na masuala mengine yaliyoelekezwa na Jaji,” akasema Bw Sossion.
Alisema kuwa muungano huo hautabembeleza TSC kuhusiana na utekelezaji wa amri hizo na kuongeza kuwa unalenga kukutana na mwajiri leo kwanza.
Aidha, alisema walimu hawako tayari kuchezewa shere na mwajiri wao jinsi hali imekuwa awali na kuapa kugoma endapo TSC itakata rufaa.
“Knut haitaruhusu mipango fiche ya TSC kutoheshimu amri za Mahakama. Wakienda Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi, walimu watagoma,” Bw Sossion akasema.
Bw Sossion alikuwa akizungumza katika shule ya upili ya wavulana ya Tenwek, katika Kaunti ya Bomet Jumamosi.
Muungano wa Knut unataka kuwe na maelewano katika sekta ya elimu kwa kutekeleza amri ambazo korti ilitoa, ili shughuli za masomo ziendelee bila kuathiriwa nchini.
“Maafisa wote wa Knut ambao walihamishwa na TSC kwa lengo la kuwaathiri warejeshwe katika shule zilizoko ndani ya maeneo yao ya uwakilishi mara moja,” akasema Bw Sossion.
Katibu huyo aliongeza kuwa TSC inafaa kufika bungeni mara moja ili kuomba ufadhili wa pesa zaidi, kuwezesha utekelezaji wa upandishaji vyeo walimu 50,000 ambao wamecheleweshwa kupandishwa ngazi, pamoja na wengine wengi.
“TSC itafute pesa mara moja kufadhili upandishaji vyeo wa walimu. Waongee na bunge ili watafutiwe pesa. Knut iko tayari kuketi na mwajiri wa walimu kuwezesha utekelezaji huo,” akasema Bw Sossion.
Knut ilieleza korti kuwa walimu wanafaa kupandishwa vyeo kulingana na muda ambao wamehudumu, kiwango cha masomo na utaalamu, nafasi za kazi zilizopo na masuala mengine yanayomhusu mwalimu.
Iliambia korti kuwa walimu wengi wamekuwa katika ngazi moja kwa miaka mitano, hata baada ya kufuzu kupanda ngazi.
Jaji Ongaya aliamrisha TSC kupandisha walimu wa muungano huo ngazi kazini kulingana na sheria.
Aidha, jaji huyo alizitaka TSC na Knut kuoanisha mfumo wa kupandisha walimu ngazi na Miafaka ya maelewano ya Walimu kurejea kazini baada ya migomo (CBA), na kwamba sheria kuhusu utendakazi wa walimu ziheshimiwe.