Makala

NGILA: Tunahitaji suluhu tosha kwa sekta ya nyama nchini

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

JUMA lililopita nilihudhuria kongamano la Siku ya Ubunifu mtaani Westlands, Nairobi lililoandaliwa na kampuni ya teknlolojia ya SAP. Nlitambua mbinu tofauti za kutumia teknolojia kuokoa uchumi wa mataifa kama Kenya unaokumbwa na visiki na maovu ya aina yake.

Mtaalamu mmoja, Bw Timo Elliot kutoka Ufaransa, alieleza jinsi teknolojia ya Blockchain inatumiwa katika jimbo la California, Amerika kufuatilia samaki wanakovuliwa, mchakato mzima wa usafirishaji hadi wanapouzwa madukani.

Ilinijia akilini jinsi teknolojia hiyo inaweza kutumiwa nchini kuwalinda Wakenya dhidi ya nyama yenye kemikali ya Sodium Metabisulfite.

Tangu ufichuzi wa runinga ya NTV kuhusu uovu huu, ilichofanya Wizara ya Afya ni kuagiza idara za afya kwenye kaunti kupima nyama katika maduka ya jumla, wachuuzi wa nyama na buchari kama ina kemikali hiyo.

Maswali mengi yameibuka kuhusu ubora wa vyakula tunavyopika. Mjadala bado unaendelea, lakini hakuna yeyote aliyependekeza mbinu madhubuti ya kuhakikisha nyama inayoliwa nchini ni salama.

Teknolojia ya Blockchain imethibitishia ulimwengu jinsi inaweza kuwatia adabu wanadamu waovu wanaokiuka maadili ya kijamii na kutenda uhuni kama kutia nyama sumu.

Huu ndio ubunifu ambao, kwa ushirikiano wa sekta ya umma na ile ya kibinafsi, na ikiunganishwa na sayansi ya data, itaweza kung’oa mtindo huu kutoka usambazaji na mauzo ya nyama.

Utaweza kutambua mambo yote yaliyotendeka kuanzia wakati mnyama alipochinjwa hadi wakati nyama yake inapikwa.

Taarifa kuhusu aina ya mnyama, aliyeichinja, ilipochinjiwa, wakati wa kuchinjwa, uzani, umri, afya yake, mnunuzi, bei, mbinu ya uchukuzi, kemikali zilizotumiwa kuhifadhi nyama, na mahali nyama inauziwa zinaweza kufuatiliwa kupitia Blockchain.

Data hii ikithibitiwa na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs), Wizara ya Afya na Shirika la Kuetetea Haki za Wakeja (Cofek), itasaidia pakubwa wakati huu ambapo wateja wanahitaji kuwa na imani ya bidhaa wanazonunua.

Wakenya hawafai kutishwa na kemikali za sulphite pekee, kuna baadhi ya nyama na bidhaa kutokana na nyama ambazo huwekwa stika zisizo, huku ripoti nyingi zikichapishwa kuhusu uchinjaji na uuzaji wa nyama ya wanyama kama punda, pundamilia na sokwe. Hizi ni nyama ambazo hazikaguliwi kabla ya kuuzwa na huweza kueneza magonjwa.

Pia, kwa kuwa teknolojia hii inawaondoa mabroka kwa sekta ya nyama, bei ya nyama itaweza kushuka na kuwapa Wakenya wa pato la chini fursa ya kufurahia minofu.

Tunaposubiri matokeo ya uchunguzi wa maabara tuliyoahidiwa na serikali, ni wakati wa kuifikiria Blockchain kama suluhu mwafaka itakayoziba mianya hii kabisa.

Bw Ngila ni mhariri wa tovuti ya taifaleo.nation.co.ke na mwanahabari wa teknolojia