• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Gharama ya umeme kupanda mwishoni mwa Machi

Gharama ya umeme kupanda mwishoni mwa Machi

Na BERNARDINE MUTANU

GHARAMA ya matumizi ya umeme inatarajiwa kupanda juu zaidi mwezi huu.

Hii ni baada ya Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) kuongeza kiwango cha ada ya mafuta katika kuzalisha umeme.

Hii ni licha ya kuwa gharama ya umeme imekuwa ikipanda katika muda wa miezi kadhaa sasa kutoka mwaka jana.

Hali hiyo ilitokana na kupungua kwa kiwango cha maji ya kuzalisha umeme kwa sababu ya ukame. Ada ya mafuta imepanda hadi Sh5.35 kwa kila kizio cha matumizi.

Agosti 2017, kiwango hicho kilikuwa ni Sh2.85. Ongezeko hilo linatokana na kuwa umeme unazalishwa kwa kutumia dizeli badala ya maji.

ERC ilitangaza hilo Ijumaa katika notisi kuwatahadharisha watumiaji wa umeme kutarajia kiwango cha juu cha bili.

Lakini kutokana na ongezeko la maji kwa sababu ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha, huenda kiwango hicho kikapungua katika muda wa miezi kadhaa ijayo.

You can share this post!

Barclays yazindua apu kuwapa wateja mikopo

Majumba 1,437 jijini Nairobi ni hatari kuishi – NCA

adminleo