• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Polisi huyu amenishtaki kwa kumnyima asali, kidosho aambia mahakama

Polisi huyu amenishtaki kwa kumnyima asali, kidosho aambia mahakama

Mary Wanjiru Ndung’u akiwa kortini Machi 20, 2018. Picha /RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

KIPUSA aliyeshtakiwa kwa kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi alimwaga mtama mahakamani Jumanne akisema “nilifikishwa kortini kwa vile nilikataa kumuonjesha afisa huyo tunda la Edeni.”

“Mheshimiwa, nimeshtakiwa sio kwa sababu nilikosa bali ni kwa sababu nilikataa kushiriki ngono ndani ya seli na afisa wa polisi katika kituo cha Central, Nairobi,” alifichua Mary Wanjiru.

Bi Wanjiru aliyekuwa ameshtakiwa kwa kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi, Konstebo Francis Maina, alizamisha dau la afisa huyo wa kulinda usalama na sasa polisi huyo anachanguzwa kwa lengo la kumfungulia mashtaka ya kumpiga na kumjeruhi mahabusu.

Kuthibitisha alipokea majeraha,  Bi Wanjiru alipelekwa katika afisi ya hakimu mkuu Francis Andayi na kuvua nguo akakaguliwa na karani wa mahakama Bi Faith Ngigi.”

“N kweli mshtakiwa yuko na majeraha usoni , shavu jeusi chini ya jicho, uvimbe kwenye paja la kushoto na matako yana majeraha,” alisema Bw Andayi.

Ilibidi korti isitishe kesi yake kwa muda kumwezesha atulie. Alilia mpaka macho yakavimba.

Kidosho huyo mwenye umri wa miaka 25 aliendelea kusema , “…baada ya kukataa na tunda langu nilichapwa kwa bao kwa makalio, mikononi na mapajani na afisa huyo aliyekuwa amepandwa na mori nilipokataa kumtimizia mahitaji yake ya kimwili.”

Wanjiru alifichua kwamba alizuiliwa tangu Jumamosi usiku hadi Jumanne kwa kukataa kumvulia chupi Konstebo Francis Maina.

 

Polisi achunguzwe

Wanjiru alionyesha mahakama majeraha aliyopata kisha hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Francis Andayi akaamuru afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Kilimani (OCS) amchunguze Konstebo Maina na kuwasilisha ripoti kortini Jumatano.

Bw Andayi aliamuru OCS huyo achunguze madai kwamba mshtakiwa huyo aliporwa Sh4,500, simu mbili za rununu na kitambulisho.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alisema, “adai haya dhidi ya afisa huyo wa polisi ni mabaya mno. Uchunguzi wa kina wapasa kufanywa ndipo ukweli ubainike.”

“Lakini ulikamatwa lini?”Andayi alimwuliza.

 

Kichapo

“Jumamosi saa sita na nusu usiku. Nilikuwa nimetoka sherehe kisha tukakosana na rafiki yangu wa kiume nikaenda kumripoti katika kituo cha polisi cha Central. Badala ya kunisaidia Konstebo Maina aliniambia nishiriki ngono naye. Nilikataa. Alinipiga sumbwi la uso na kunisukuma korokoroni.”

Andayi alimwachilia Wanjiru kwa dhamana ya Sh30,000 pesa taslimu na kuamuru arudishwe kortini Jumatano baada ya kuandikisha taarifa ya matukio hayo kwa OCS Kilimani.

Vile vile OCS huyo aliamriwa ampeleke Hospitali Kuu ya Kenyatta na kuwasilisha ripoti kortini.

You can share this post!

Waiguru na Karua wabanana mahakamani

Uchawi wazidi kanisani huku waumini wakiamini nguvu za giza...

adminleo