Habari Mseto

Atwoli akasirishwa na hatua ya TSC kukata mishahara ya walimu

August 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Bw Francis Atwoli amekasirishwa na hatua ya Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) ya kukata mishahara ya walimu zaidi ya 100,000 ambayo imeibua hisia kali.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Katibu Mkuu huyo alitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria hadharani.

“Hatua ya TSC ni sawa na ufisadi, ukiukaji sheria, ni kinyume na katiba na sheria zetu mbalimbali. Kulingana na Muungano wa Kimataifa wa Wafanyakazi (ILO) na Kifungu cha Katiba kuhusu Malipo ya Wafanyakazi, mtu yeyote hawezi kupunguza mshahara wa mwajiriwa bila idhini yake.”

Akaongeza: “Sheria hizo zinapiga marufuku hatua yoyote ya kukata mishahara na marupurupu ya mfanyakazi hivyo basi kumlinda kutokana na kupunguziwa mshahara kinyume na sheria.”

Alifafanua kwamba ilikuwa kinyume na sheria za ILO kukiuka mkataba wa kuongeza mishahara ya wafanyakazi baada ya kuidhinishwa na Mkataba kuhusu Malipo ya Mishahara (CBA).

“Mfanyakazi anapopatiwa nyongeza ya mshahara kupitia CBA ambayo imesajiliwa kisheria, nyongeza hiyo haiwezi kurejeshwa. Hivyo basi TSC inapaswa kukoma kukiuka haki za walimu kupitia hatua kama hizo zisizofaa kisheria,” alisema,

Aidha, Bw Atwoli alitoa wito kwa serikali, Muungano wa Kitaifa wa Walimu (KNUT) pamoja na TSC kukomesha mvutano baina yao akisema hali hiyo ilikuwa ikitoa picha mbaya kuhusu Kenya kama taifa lisilojiweza kisiasa, wala kuwa na mifumo ya mahusiano ya kiviwanda inayoweza kutatua migogoro kati ya miungano ya wafanyakazi na usimamizi.

“COTU (K) inapinga vikali juhudi hizi kwa sababu si za haki. Hii ni sawa na kuwatia hofu na kuwahangaisha walimu kwa sababu ya kujiunga na muungano. Ni jambo lisilofaa kabisa kwa pande husika kuvuana nguo hadharani kila mara kupitia magazeti. Haijawahi kutendeka kwingineko kwamba baada ya mwajiri kumpa mfanyikazi nyongeza ya mshahara kupitia mkataba wa CBA jinsi TSC ilivyofanya, anaweza tena kubadilika na kuanza kutoa vitisho vya aina yote. Ni ukiukaji wa kanuni za mahusiano mema ya kiviwanda,” alisema, huku akiishauri TSC kwamba CBA inajumuishwa katika sheria nchini na inapaswa kuzingatiwa kikamilifu.

Magazeti

Bw Atwoli alionya pande husika dhidi ya kuendesha mahusiano yao ya kiviwanda kupitia mahakama na magazeti, huku akiomba Waziri wa Elimu Bw George Magogha na Waziri wa Leba Balozi Ukur Yattani, kuandaa kikao kinachojumuisha pande tatu: Muungano wa Kitaifa wa Waajiri (FKE), COTU (K) na Wizara ya Leba, kwa lengo la kutoa mwelekeo kwa TSC na KNUT.

“Tukikosa kufanya hivyo, ninaona kuvurugika kwa taaluma ya ualimu hali ambayo bila shaka itaathiri mfumo wetu wa elimu,” alionya.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya TSC kuwarusha nje walimu 103, 624 katika Awamu ya Tatu ya nyongeza ya mishahara ya jumla ya kiasi cha Sh13 bilioni, katika hatua iliyoibua ghadhabu miongoni mwa walimu kote nchini.

Walimu walioathirika pakubwa ni wanaoshikilia nyadhifa za usimamizi na ambao pia ni wanachama wa KNUT.

Isitoshe, walimu wanachama wa KNUT walipata pigo kuu baada ya TSC kuanza mchakato wa kutwaa mabilioni ya hela walizolipwa tangu miaka miwili iliyopita wakati mkataba wa malipo ulipoanza kutekelezwa.

KNUT iliathirika pakubwa hasa baada ya kubainika kwamba TSC haikuwa ikikata kiasi cha Sh140 milioni kila mwezi, hali iliyotishia kulemaza shughuli za muungano huo wa walimu.