Habari Mseto

Wakulima wakasirishwa na upungufu wa mbolea

March 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

WAKULIMA wa nafaka kutoka eneo la Kaskazini mwa Rift Valley wamelalamikia uhaba wa mbolea msimu huu wa upanzi.

Wakihutubia wanahabari katika bohari ya bodi ya mazao na nafaka (NCPB) mjini Eldoret, walisema uhaba huo wa mbolea unahatarisha kupatikana kwa chakula cha kutosha.

“Kunapokuwa na uhaba wa mbolea kama tunaoushuhudia sasa, matokeo yake ni kuwa wakulima hawatavuna chakula cha kutosha.

Hili ni jambo litakalosababisha baa la njaa kama inayoshuhudiwa hata sasa katika baadhi ya maeneo ya nchi,” akasema Mkurugenzi wa shirikisho la Wakulima (KFA), Bw Kipkorir Menjo.

Wakulima wengi ambao walifika katika bohari ya NCPB mjini Eldoret kununua mbolea, walipigwa na butwaa baada ya kufahamishwa kuwa maghala hayo hayakuwa na mbolea.

Kinaya ni kwamba, mbolea ya kunyunyizia mimea aina ya CAN ndiyo inapatikana badala ya mbolea ya DAP.

Wakulima hao walitaka kujua sababu ya mbolea hiyo kukosekana wakati huu, na wakasema wanashuku huenda kuna njama ya kuficha mbolea hiyo ili wafanyibiashara wachache wauzie wakulima kwa bei ghali.

Bw Menjo alitaka serikali kuelezea wakulima ilikokwenda mbolea ambayo ilidaiwa kufika katika bandari ya Mombasa mwezi uliopita.

“Tuliambiwa shehena ya mbolea imefika Mombasa, mbona mbolea hii haijafika,” alishangaa Bw Menjo. Vile vile wakulima hao walilamikia msongamano na foleni ndefu za kuuza mahindi katika NCPB mjini humo.

Walitaka shirika hilo kuharakisha mchakato wa kupakua mahindi.

Mbali na changamoto hiyo wakulima husika walitaka kujua ni kwa nini serikali inaruhusu mahindi kutoka nchi jirani ya Uganda kuuzwa nchini ilhali wakulima wa nchini wangali na mahindi ambayo walivuna mwaka jana.