• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
SIHA NA LISHE: Mazoezi yanaenda sambamba na mlo

SIHA NA LISHE: Mazoezi yanaenda sambamba na mlo

Na MARGARET MAINA

[email protected]

NI muhimu kufahamu jinsi vyakula vinavyoweza ama kuimarisha au kuharibu matokeo ya mazoezi.

Unapotaka kuwa na afya njema, unastahili kufanya mazoezi na ule vizuri.

Huwezi kuafikia malengo ya kuwa na afya bora bila kuzingatia mazoezi na lishe bora kwa wakati mmoja. Maana yake ni kwamba, hata kama utafanya mazoezi mara kwa mara, lakini lishe yako ikawa mbovu, basi usitegemee kupata mafanikio makubwa ya malengo yako.

Watu wengi hufanya mazoezi, lakini huishia kulalamika kutokuafikia malengo waliyojipangia.

Hapa zipo mada kadha za kuelekeza mwenye malengo ya kuwa na afya njema. Mada zimezingatia yale yasiyofaa kisha uchanganuzi ukabainisha kinachostahili kufanyika.

Kula chakula kingi mara baada ya mazoezi

Kwa kawaida unapofanya mazoezi mwili hutumia nguvu nyingi. Hii ni mojawapo ya sababu zinazokufanya uhisi njaa na hamu ya kula mara baada ya kufanya mazoezi. Jizoeshe tabia ya kula mlo mdogo badala ya kula chakula kingi kwa sababu hurudisha mwilini nishati-lishe (calories) ulizozitumia wakati wa mazoezi, hivyo ‘kufuta’ faida ulizokuwa umezipata kwa kufanya mazoezi.

Kula chakula kisichofaa baada ya mazoezi

Nguvu au nishati-lishe inayokuwa imetumiwa wakati wa mazoezi hukufanya uwe na hamu ya vyakula vyenye sukari, mafuta na wanga.

Hii inatokana na mabadiliko ya vichocheo au homoni (hormones) zinazoendana na utumiaji wa nishati-lishe mwilini wakati wa mazoezi. Hii ndiyo sababu ya watu wengi kuwa na hamu na vyakula vya aina hii. Lakini epuka vitu kama soda, juisi zenye sukari nyingi na baadala yake kula mlo wenye sukari ya asili, kama vile juisi ya matunda isiyoongezwa sukari. Pia kula mlo wenye kiasi kikubwa cha protini ili kuusaidia mwili kurudi katika hali yake.

Kula chakula kingi zaidi ya kiasi cha mazoezi unayofanya

Watu wengi hudhani kwamba, kwa kuwa wanafanya mazoezi hawana haja ya kujali kiasi na aina ya chakula wanachokula. Ikumbukwe kwamba kinachotakiwa ni uwiano kati ya nishati-lishe inayoingia na ile inayotoka mwilini.

Nishati-lishe huingia mwilini kwa njia ya chakula, na hutumika au kutoka mwilini kwa kufanya mazoezi. Kutokana na malengo mbalimbali ni muhimu kufahamu jinsi ya kufikia uwiano utakaokufanya ufaidike.

Kwa mfano, endapo lengo lako ni kupungua uzani, ni sharti utumie nishati-lishe nyingi zaidi ya zile unazoingiza mwilini.

Maana yake ni kwamba, kiasi na kiwango cha mazoezi kizidi kiasi cha chakula unachokula. Ukikosea uwiano huu huwezi kufaidika na mazoezi.

Kutumia kiasi kidogo cha protini na wanga kwa wingi

Mafuta hujengeka na kuongezeka mwilini kutokana na kiasi kikubwa cha nishati-lishe kinachoingia mwilini kama chakula.

Vyakula vya wanga na vile vya mafuta hutoa nishati-lishe nyingi zaidi ya vyakula vya protini. Ifahamike pia kwamba uyeyushaji wa vyakula vya protini hutumia nishati-lishe nyingi hivyo kusaidia kutumia nishati-lishe ya ziada mwilini.

Kwa maana hiyo, pamoja na kufanya mazoezi, vyakula vyenye protini nyingi na wanga kidogo husaidia kuzuia ongezeko la mafuta mwilini.

Kunywa pombe kupita kiasi

Pombe ina nishati-lishe nyingi. Kwa maana hiyo, unywaji pombe kupita kiwango kilichoshauriwa huchangia katika kuongeza mafuta mwilini. Hata kama unafanya mazoezi kwa kiwango kikubwa, kunywa pombe kupindukia kutarudisha nyuma juhudi zako.

Kula chakula kingi chenye wanga usiku

Wengi wetu hupumzika usiku. Kwa maana hiyo, hatuhitaji nguvu nyingi mwilini. Kula kiasi kikubwa cha wanga hutupa nguvu ya ziada, ambayo hatuitumii.

Nguvu hii ya ziada hutunzwa mwilini kama mafuta. Kwa maana hiyo, hata kama utakuwa ulichoma mafuta ya kutosha wakati wa mazoezi, kula chakula kingi cha aina ya wanga wakati wa usiku hupoteza juhudi zako za mazoezi.

You can share this post!

MSHAIRI WETU: Wangu Kanuri almaarufu ‘Malenga wa...

Duale: Uchaguzi mkuu 2022 ni kinyang’anyiro cha Ruto...

adminleo