HabariSiasa

Pigo kwa Jubilee Mariga kufungiwa nje na IEBC

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

MGAWANYIKO ndani ya Chama cha Jubilee kuhusu ugombeaji wa ubunge Kibra ulizidi kudhihirika Jumanne wakati wakuu wa chama hicho walikosa kujitokeza kumkabidhi rasmi Bw McDonald Mariga vyeti vya uwaniaji, na kuchangia kufungiwa nje kwa mwaniaji huyo na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Tofauti na vyama vingine vya kisiasa ambako wagombeaji walilakiwa na wakuu wa vyama baada ya kuteuliwa kuwania wadhifa huo, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, hawakuwepo katika makao makuu ya Jubilee Bw Mariga alipopewa vyeti.

Badala yake, shughuli hiyo ilisimamiwa na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju akiandamana na wanasiasa wengine wa chama hicho hasa wa mrengo wa Tangatanga unaomuunga mkono Dkt Ruto.

Tangu kuteuliwa kuwa mwaniaji wa Jubilee, Bw Mariga hajawahi kukutana na Rais Kenyatta ambaye ni kiongozi wa chama hicho.

Duru zilisema, uamuzi wa kuwasilisha mwaniaji wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra ulifanywa na Dkt Ruto kwa lengo la kumpinga Bw Odinga.

Ripoti zilisema Rais Kenyatta alikataa mwaliko wa naibu wake aliyemtaka aende kumkabidhi Bw Mariga cheti cha uteuzi katika makao makuu ya chama cha Jubilee.

Viongozi wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Kieleweke unaopinga mienendo ya Tangatanga, wakiwemo Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny na Mbunge Maalumu Maina Kamanda wanadai kuna baadhi ya watu ndani ya Jubilee wanalenga kusambaratisha uhusiano mwema uliopo baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa kusimamisha mwaniaji Kibra.

“Naibu wa Rais anajua kwamba hatashinda kiti cha Kibra na lengo lake kuu ni kutaka kuzua uhasama kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bw Kamanda.

Wakati huo huo, Bw Tuju pia amethibitisha kuwa Rais Kenyatta hatashiriki katika kampeni za ubunge Kibra.

Viongozi wa Vyama vya ODM, Ford-Kenya, na Amani National Congress ambavyo vina wagombeaji wanaomezea mate kiti hicho kilichoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge, Ken Okoth, wamekuwa mstari wa mbele kutafutia umaarufu wagombeaji wao.

Bw Odinga alimtangaza mbunge wa Suna Mashariki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, kuwa kinara wa kampeni za Bw Okoth katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

Bw Odinga alifanya kikao cha faragha na wawaniaji wote waliopoteza katika uchaguzi wa kura za mchujo uliofanyika Jumamosi iliyopita ili kuwapatanisha baada ya malalamishi kuibuka miongoni mwa baadhi yao awali.

Baada ya kikao hicho, wawaniaji hao walitangaza kumuunga mkono Bw Bernard Otieno Okoth, almaarufu Imran, aliyeibuka mshindi.

“Hii ilikuwa mechi ya kirafiki, hivyo hakuna uhasama kati yetu. ODM ni chama kinachozingatia demokrasia na sasa tutaunga mkono Bw Imran Okoth na tutahakikisha chama chetu kinahifadhi kiti hicho,” akasema Bw Peter Orero ambaye awali alikuwa amelalamika kuhusu udanganyifu katika kura ya mchujo.

Wawaniaji wengine ambao wamewasilisha stakabadhi zao kwa IEBC ni Eliud Owalo wa chama cha Amani National Congress (ANC), Khamisi Butichi wa Ford Kenya, Malaseh Hamida (United Green Movement) Editar Ochieng (Chama cha Ukweli chake mwanaharakati Boniface Mwangi) na Fridah Kerubo Kingara (mwaniaji wa kujitegemea).