Kamworor aweka rekodi mpya ya mbio za kilomita 21
Na GEOFFREY ANENE
BINGWA mara tatu wa Riadha za Nusu-Marathon Duniani, Geoffrey Kamworor ameweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za kilomita 21 baada ya kutwaa taji la Copenhagen Half Marathon kwa dakika 58:01 nchini Denmark mnamo Septemba 15, 2019.
Kamworor, ambaye alitumia mbio za Copenhagen kama maandalizi ya mbio za kilomita 42 za New York zitakazofanyika nchini Marekani mnamo Novemba 3 mwaka 2019, alifuta rekodi ya Mkenya mwenzake Abraham Kiptum ya dakika 58:18 iliyowekwa mjini Valencia nchini Uhispania mnamo Oktoba 28, 2018.
Amejishindia Sh1.0 milioni kwa ushindi, Sh1.0 milioni kwa rekodi ya dunia, Sh518,550 kwa rekodi mpya ya Copenhagen Half Marathon na Sh207,420 kwa kukamilisha umbali huo chini ya dakika 60. Ushuru wa asilimia 15 utatolewa katika tuzo hiyo.
Mkimbiaji huyu aliyebeba mataji ya dunia ya Half Marathon mwaka mwaka 2014, 2016 na 2018, alichupa uongozini mjini Copenhagen baada ya kilomita 11 na kujiweka pazuri kuvunja rekodi alipopita kilomita 13 kwa dakika 35:40, kilomita 15 kwa dakika 41:05 na kilomita 18 kwa dakika 49:26.
Kamworor aliingia mbio za Copenhagen akiwa na muda wake bora katika mbio za kilomita 21 wa dakika 58:54.
Mbali na kuvunja rekodi ya dunia, muda wa Kamworor pia alifuta rekodi ya Copenhagen Half Marathon ya dakika 58:40 iliyowekwa na Mbahraini Abraham Cheroben, ambaye ni mzawa wa Kenya, mwaka 2017.
Kamworor alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Benard Kipkorir Ng’eno (dakika 59:16), Muethiopia Berehanu Tsegu (59:22) na Wakenya Edwin Kiptoo (59:27), Amos Kurgat (59:37), Philemon Kiplimo (59:57) na Shadrack Koech (saa 1:00:12), mtawalia.
Kabla ya Kamworor, Wakenya Bedan Karoki, James Wangari na Daniel Kipchumba walikuwa wametwaa mataji ya Copenhagen mwaka 2015, 2016 na 2018, mtawalia.
Taji la wanawake limenyakuliwa na Muethiopia Birhane Dibaba kwa saa 1:05:57 akifuatiwa unyounyo na Mkenya Evaline Chirchir (1:06:22), Dorcas Tuitoek (1:06:36), mtawalia. Purity Rionoripo anasalia Mkenya wa pekee kushinda taji la wanawake la Copenhagen Half Marathon. Aliibuka mshindi mwaka 2015.